Kampuni ya Airtel Africa imetangaza kufikisha jumla ya wateja milioni 166.1 katika mataifa 14 ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, katika mataifa 14 ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, kulingana na tathmini iliyofanyika mwisho wa mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2025.
Idadi hiyo inaashiria ongezeko la asilimia 8.7, likichochewa na uwekezaji unaolenga kuimarisha ujumuishaji wa kidijitali na kupanua huduma za kifedha kupitia simu.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, wateja wa huduma za intaneti wameongezeka kwa asilimia 14.1 hadi milioni 73.4, huku matumizi ya data kwa kila mteja yakipanda kwa asilimia 30.4. Wateja wa huduma ya Airtel Money pia wameongezeka kwa asilimia 17.3 na kufikia milioni 44.6, huku thamani ya miamala ikifikia dola bilioni 145 kwa mwaka.
“Mkakati wetu unaoangazia uzoefu bora kwa mteja na upanuzi wa miundombinu umeendelea kuzaa matunda,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar. “Tumepanua mtandao wetu, kuboresha majukwaa yetu ya kidijitali, na kuongeza idadi ya vituo vya kutoa huduma ili kusaidia ujumuishaji wa kifedha.”
Licha ya changamoto za mabadiliko ya sarafu katika baadhi ya masoko, Airtel imetangaza faida ya dola milioni 328 baada ya kodi, tofauti na hasara ya dola milioni 89 mwaka uliopita. Kampuni pia imetangaza gawio la senti 6.5 kwa kila hisa kwa mwaka mzima.
