Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kukerwa na utaratibu wa kugharimia miradi kwa kuomba misaada nje ilihali inaweza kugharimiwa na fedha za ndani.
Sambamba na hilo, amesema masharti yanayotolewa na wahisani hayana msingi hivyo ni wakati wa taifa kutegemea zaidi makusanyo ya ndani zaidi kuliko misaada kutoka nje kugharimia miradi mbalimbali.
Rais Samia amesema hayo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wakati akifungua jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu lililogharimu Sh bilioni 9.483.
Alisema ili kuondokana na hali hiyo, watumishi wa TRA wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya serikali iliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.
Aliongeza kuwa ni dhamira ya serikali kutumia fedha za ndani katika kugharimia miradi mbalimbali isipokuwa miradi mikubwa kama Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Rais Samia aliwakumbusha watumishi wa TRA kuwa ili kutimiza malengo ya ukusanyaji wa mapato, ni lazima wakusanye kodi kwa maelewano bila kutumia nguvu ili walipakodi wote waone ni wajibu wao kulipa kodi kwa hiyari.
Alisema wafanyabiashara wote hawapaswi kuwa adui wa TRA bali wanatakiwa kuwa rafiki ili mwenye uwezo alipe kwa hiyari na mwenye madeni aitwe wakae pamoja wazungumze namna ya kulipa, ikibidi ndio matumizi ya nguvu yatumike.
“Zamani ukisikia TRA, kila mtu alitamani kwenda huko. Ukikaa miezi mitatu, sita umenona suti nzuri unang’aa lakini sasa ni TRA ya kukusanya kwa ajili ya nchi yetu hilo nawapongeza sana,” alisema.
Aliwaeleza kuwa enzi za kuvaa suti na kupandisha mabega kwa watumishi wa TRA bila kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao imepitwa na wakati na sasa kinachotazamwa ni juhudi na bidii katika ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya nchi.
“Uwepo wa majengo haya umeboresha hali ya utendaji kazi, nimeona majengo ni mazuri mno, lakini ndani kuna vitendea kazi vya kisasa. Kuna mifumo madhubuti inayowapa urahisi wa kufanya kazi zenu,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, hakuna sababu sasa ya kutofikia malengo ya ukusanyaji wa kodi kwani ameidhinisha wafanyakazi wapya zaidi ya 1,000 kujiunga na timu ya TRA.


Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amesema huduma za usafiri zinazotolewa kwenye mradi wa mabasi yaendayo haraka mkoani Dar es Salaam zitaanza kuwa bora mwishoni mwa Julai mwaka huu baada ya serikali kupata kampuni nne binafsi zitakazotoa huduma kwenye barabara hizo.
Kauli hiyo ameitoa Dar es Salaam wakati akizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani humo ikiwa ni hitimisho la kampeni hiyo katika mikoa yote 31 nchini.
Alisema serikali inatambua changamoto ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka unaotekelezwa na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambao amekiri kuwa uwezo wao wa kutoa huduma umepungua na kusababisha kero kwa wananchi.
“Serikali imebaini hilo la kuzorota kwa huduma za mabasi hayo na tumechukua hatua, Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kufuatilia hili aliamua akabidhi rasmi jambo hilo ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Majaliwa.
Alisema tangu akabidhiwe suala hilo, ni wiki mbili zimeisha na hatua kadhaa zinaendelea kuchukuliwa kubaini changamoto zilipo na suluhu yake.
Katika hilo, alisema waliamua kushirikisha sekta binafsi na wameshapata kampuni nne zitakazotoa huduma pamoja na UDART itakuwa ya tano.
Alisema kampuni ya kwanza itahudumia Barabara la Mbagala na katika hilo, mabasi 344 yataingizwa barabarani.
Kampuni nyingine itatoa huduma barabara ya Gongo la Mboto, nyingine itatoa huduma barabara za mlisho ikihusisha mabasi 150.
Nyingine itatoa huduma barabara ya Kigamboni ambayo mabasi 280 yatahusika na UDART watabaki na barabara ya Kimara Kivukoni na gerezani ambapo mabasi 277
yatahusika.
Alisema katika kipindi kifupi kijacho wananchi wanaohudumiwa na barabara hizo na nyingine zinazoendelea kujengwa wataondokana na kero hiyo ya usafiri.
“Tunaendelea na ukarabati, lengo ni kurudisha hii ya usafiri kwa viwango bora zaidi,” alisema Majaliwa.
Alisema katika uboreshaji huo, wamiliki wa daladala hawataachwa nyuma nao watahusishwa ili kufanya kazi katika mradi huo. “Tutashirikisha pia wamiliki wa daladala, hatuwezi kuwaacha, watafanya kazi,” alisema Majaliwa.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hivi sasa kiwanda cha kuchakata pamba kinajengwa ambapo kitatumika kuichakata pamba ili kutengeneza nyuzi zitokanazo na pamba.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira lakini pia pamba inayozalishwa ndani ya nchi kutumika hapa hapa nchini kuzalisha bidhaa nyingine badala ya kuisafirisha nje ya nchi kama ambavyo inavyofanyika sasa.
Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 16, 2025 baada ya kuzindua kiwanda cha kuchambua pamba pamoja na kiwanda cha kutengeneza mabomba wilayani Bariadi mkoani Simiyu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo.
“Tunajua kwamba Simiyu zao kubwa la kiuchumi ni pamba ukiacha mengine na nimshukuru mwekezaji hapa wa ndani amewaza kuongeza thamani angalau kwa hatua ya kwanza, lakini hatua ya pili sasa tutanunua kwake kuweka kwenye kiwanda ambacho tayari tumeanza kukijenga cha kutengeneza nyuzi za pamba. Tunataka kusitisha kupeleka pamba yetu kama ilivyo kwenye marobota kwa wenzetu wakatengeneze nguo na watu wao wapate kazi, tunataka pamba yetu tuitengeneze hapa hapa ili watu wetu wa Simiyu waweze kupata ajira ndani ya mkoa huu,” amesema Rais Samia

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Seif Shekalage kutuma timu ya wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kufanya ukaguzi na kuangalia kama mfumo wa Tehama unafanya kazi ipasavyo.
Jenista alitoa maagizo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu katika hospitali hiyo kisha kuzungumza na watumishi.
Alisema mfumo wa Tehama kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utoaji huduma bora za afya kwa wananchi, ikiwemo kuweka ulinzi na usalama wa miundombinu ya hospitali.
Alisema alipewa taarifa na uongozi wa hospitali hiyo kuwa wamekuwa wakitumia walinzi kufuatilia upotevu wa baadhi ya vitu, utaratibu ambao alisema umepitwa na wakati kwani kila kitu kinaendeshwa kwa Tehama.
“Hospitali hii imewekwa mifumo ya Tehama, kama mfumo wetu umeunganishwa idara zote za hospitali inakuwaje tushindwe kudhibiti mwenendo mzima wa shughuli zote zinazofanyika kwenye hospitali yetu?” Alihoji.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na utalii endelevu, sambamba na mabadiliko ya kiuchumi kutoka nchi ya kipato cha chini hadi kipato cha kati cha juu.
Mkakati huo unalenga kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya jamii na kuongeza mapato ya Taifa kupitia matumizi bora ya rasilimali za asili.
Akizungumza katika warsha ya kitaifa inayoangazia Uhifadhi na Mchango wake katika Utalii na Maendeleo ya Jamii, iliyofanyika jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana alisema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea misaada na ruzuku, bali inapaswa kuwa mshirika wa maendeleo kupitia sekta ya utalii.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na utalii unaonufaisha wananchi moja kwa moja.
Dk. Chana alibainisha kuwa licha ya mafanikio ya ongezeko la idadi ya watalii kutoka milioni 1.7 mwaka 2021 hadi milioni 5.3 mwaka 2024, na mapato kutoka dola bilioni 1.3 hadi bilioni 3.9, bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza manufaa kwa jamii. Alitoa wito kwa wataalamu na wadau kuendeleza tafiti na ubunifu katika sekta hiyo.
Warsha hiyo, iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, inalenga kujadili mbinu bora za kuendeleza utalii unaohimiza uhifadhi wa mazingira, kukuza ajira, na kuboresha maisha ya Watanzania kupitia utalii jumuishi na wa kisasa.