RAIS wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva ametangaza maobolezo ya siku saba kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Francis, kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani.
“Ulimwengu umepoteza sauti ya muhimu ya heshima na hisani,” alisema Rais Lula da Silva.
Brazil ni nchi ambayo ina idadi kubwa zaidi ya waumini wa Kanisa Katoliki ambao watapatiwa fursa kuungana katika kumuenzi kiongozi wao ambaye alifariki dunia mapema Jumatatu katika makao makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, akiwa na umri wa miaka 88.
Waumini wa Kanisa Katoliki nchini humo walijitokeza kwa wingi kushiriki ibada za kumuombea Papa Francis, huku wakitafakari michango yake kwenye imani ya Kikristo na juhudi zake za kuleta umoja na upendo miongoni mwa watu.
Kwa mujibu wa ripoti za Vatican, Brazil ina wakazi wapatao milioni 182 na inachukuliwa kuwa nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi duniani, kati ya jumla ya watu bilioni 1.4 walio sehemu ya Kanisa Katoliki.
Maombolezo haya yanatarajiwa kuleta faraja kwa waumini wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa kiongozi aliyejulikana kwa msingi thabiti wa amani na upendo.
