Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Chama cha kiliberali cha Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney kimeshinda uchaguzi wa Bunge na hivyo kujipatia muhula mwengine madarakani.
Lakini haijawa wazi ikiwa chama hicho kitapata idadi kubwa ya wabunge na kukipiku chama cha wahafidhina kinachoongozwa na Pierre Poilievre. Canada imefanya uchaguzi wake wa bunge Aprili 28, 2025 ili kuamua chama kitakachoiongoza Serikali ijayo chini ya kiwingu cha mivutano na Taifa jirani na lenye nguvu za kiuchumi Marekani. Wapiga kura walikuwa wanaamua kati ya kukirejesha madarakani chama cha Kiliberali chini ya mwanasiasa Mark Carney au kuwachagua wahafidhina wanaoongozwa na mwanasiasa Pierre Poilierve .
Zaidi ya raia milioni 28 wa Canada waliorodeshwa kwenye daftari la wapiga kura. Uchaguzi huu ulishuhudia pia rekodi ya raia milioni 7.3 waliofanikiwa kupiga kura ya mapema. Baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifungwa usiku wa jana na kura kuanza kuhesabiwa.
Pia, uchaguzi huo ulionekana kuwa muhimu kwa rais wa Marekani Donald Trump ambaye kama kawaida yake aliandika kwenye mitandao ya kijamii na kuwatolea wito raia wa Canada kumchagua kiongozi ambaye atakuwa na busara na ujasiri wa kuifanya nchi hiyo kuwa jimbo la 51 la Marekani akidai kuwa itakuwa fursa kubwa kwa Canada.
Hata hivyo, wakati wa kampeni, wagombea wakuu katika uchaguzi huo ambao ni Mark Carney wa chama cha Kiliberali na mhafidhina Pierre Poilierve hawakuzungumzia suala hilo la Canada kuwa jimbo la Marekani, fikra ambayo hata hivyo inapingwa vikali na idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo.