Wabunge wa Bunge la Ulaya wamejadili kwa dharura masuala ya kisiasa nchini Tanzania wakilenga kuhusu kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu na hatari ya hukumu yake iwapo atapatikana na hatia ya uhaini ambapo wametoa wito kwa Mamlaka za Tanzania kumuachia Lissu na kuweka mazingira rafiki kwa Vyama vya upinzani ikiwemo CHADEMA kushiriki uchaguzi wa mwaka huu 2025.
Bunge hilo limetoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuirejesha CHADEMA katika mchakato wa kisiasa na kuhakikisha kwamba haki za Binadamu, uhuru wa kujieleza, na haki ya kupata haki Mahakamani na pia Serikali ya Tanzania imepewa wito wa kufuta adhabu ya kifo na kubadilisha hukumu zote za kifo.
Baada ya mjadala huo wa jana May 07,2025, Wabunge wa Ulaya wataandaa na kupiga kura juu ya azimio maalum lenye rejea 2025/2690 (RSP) leo May 8, 2025 kuhusu mjadala huo wa kesi ya Lissu ambapo Bunge hilo limetaka taarifa yao iwasilishwe kwa Serikali na Bunge la Tanzania, Umoja wa Afrika na Mwakilishi Mkuu wa Sera za Mambo ya Nje wa EU, kwa lengo la kuanzisha mashauriano ya dhati na yenye matokeo ya kweli kwa maendeleo ya kisiasa ya Tanzania.
Lissu anakabiliwa na mashtaka mawili ambapo moja ni la uchochezi na jingine ni la uhaini ambalo adhabu yake ni kunyongwa endapo atakutwa na hatia.