Bunge limepitisha kwa kishindo jumla ya Sh Trilioni 2.439 bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuwezesha utekelezaji wa malengo ya wizara na taasisi zake yaliyoanishwa kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Bajeti hiyo imepitishwa kwa asilimia 100 leo Mei 13 ikiwa na mchanganuo wa Sh bilioni 688.6 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Sh bilioni 635.2 ni kwa ajili ya mishahara na Sh bilioni 53.3 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Utekelezaji wa bajeti hiyo utajikita zaidi katika maeneo matano ya vipaumbele ambayo ni i) kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya sheria, Uandaaji wa miongozo, na utoaji wa mafunzo, ii) Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya Amali katika shule za sekondari na vyuo vya Amali, iii) Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya Amali, Msingi, Sekondari na Ualimu, iv) Kuongeza na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na v) Kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, Matumizi ya Sanyansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.
Wabunge wamempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda (Mb) kwa utulivu wa kiutendaji katika wizara yake na mshikamano alionao na watendaji wote wa Wizara na kumsihi kusimamia kwa weledi mkubwa wizara hiyo ambayo ni msingi wa maendeleo ya nchi.
Kati ya fedha zilizopitishwa, zaidi ya Sh trilioni 1.7 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Sh 1.186 ni fedha za ndani na Sh 560.8 ni fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO imeidhinishiwa jumla ya Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Mishahara ni Sh bilioni 1.5 na Matumizi Mengineyo ni Sh bilioni 1.7
