Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tanzania Bara John Heche amewataka Wanachama wa Chama hicho kutotishwa wala kubabaishwa na walioshindwa mapambano na kuondoka kisa CHADEMA haishiriki uchaguzi bila mabadiliko kufanyika ambapo amesema Chama hicho kilianzishwa ili kuwaletea Watanzania mabadiliko na sio kutimiza ndoto za Watu kuwa Wabunge hata kupitia uchaguzi usio huru na haki.
Akiongea na Wakazi wa Sengerema Mkoani Mwanza leo Mei 12,2025, Heche amesema “No reforms no election ndio msimamo wa nchi, sasa wanaopotoka kuna wakati miongoni mwetu tulikuwa nao kwenye safari hii wameshindwa mapambano, wasitutishe, wanatuambia kwamba eti ndoto zao zinakatishwa kwa sisi kutoenda kwenye uchaguzi wa kuua Watu”
“Hiki Chama hakikuanzishwa kwa ajili ya ndoto ya Mimi Heche kuwa Mbunge, kilianzishwa kwa ndoto ya kuwaletea Watanzania mabadiliko, sio ndoto ya kukufanya uwe Diwani au Mbunge, hiki ni Chama cha ndoto ya Watanzania kurudisha nchi yao kwenye mikono yao, wasiwatishe, msibabaike, safari lazima iendele” amesema Heche
