Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amefanya ziara ya kukagua hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kukipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Mama Ngoma kuwa hospitali ya ngazi ya juu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mollel amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa, na amesisitiza umuhimu wa mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma kwa wananchi. “Tupo hapa kuhakikisha kilichoelekezwa na Waziri Mkuu kinatekelezwa kwa vitendo. Serikali haishindani na sekta binafsi bali tunashirikiana kutoa huduma bora kwa jamii,” amesema Dkt. Mollel.
Kwa upande wake, Profesa Ngoma ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa kituo hicho katika jamii na kukipa kipaumbele. “Hili si jambo kwa ajili ya mtu mmoja, ni kwa manufaa ya wananchi wote wa eneo hili na maeneo ya jirani,” amesema Profesa huyo..
Uwepo wa Hospitali ya Mama Ngoma katika eneo la Kwangoa umetajwa kuwa muhimu kutokana na umbali wa hospitali ya wilaya, hivyo kusaidia kupunguza gharama za Serikali na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.