Spika wa Bunge na Rais wa 31 wa Muungano wa Mabunge Duniani IPU ,Dkt. Tulia Ackson, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, mkoani Pwani, kuacha ushindani na makundi ndani ya chama ambao unaweza kusababisha madhara kwa kutoa upenyo kwa upinzani wakati wa Uchaguzi.
Akizungumza April 25, 2025 na viongozi mabalozi pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kibaha Mjini, kutoka kata ya Viziwaziwa Kongowe na Msangani wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, Dkt Tulia ambae alikuwa mgeni maalum aliongeza kuwa waachane na ushindani ili kukiimarisha Chama.
"Msifanye ushindani wa namna ya Yanga na Simba, bali muangalie viongozi ambao wanaonekana kufanya kazi kwa manufaa yenu, wanaccm lazima tuwatupe mbali wapinzani, utekelezaji unaonekana kwa macho, Rais Samia Suluhu Hassan anastahili heshima kwa kumpa kura za ushindi na sio za kinyonge." alisema Dkt. Tulia