Hatua hiyo inajiri zaidi ya miezi miwili tangu ulipofanyika uchaguzi mwishoni mwa mwezi Februari.
Merz ambaye alikuwa mgombea wa vyama hivyo viwili vilivyopata ushindi mwembamba kwenye uchaguzi huo, atachukua rasmi wadhifa wa ukansela pale bunge la taifa, Bundestag, litakapopiga kura mjini Berlin ili kumuidhinisha.
Ataongoza serikali ya mseto na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha SPD, ambacho ni cha kansela anayeondoka, Olaf Scholz.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano ya kuunda serikali, Merz amesema anatumai watamudu kuiongoza Ujerumani kwa njia madhubuti na kushughulikia changamoto zinazolikabili taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.