Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO) ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imesema kuwa imewekeza vya kutosha katika matumizi ya teknolojia inayotumia akili mnemba (AI) kwa ajili ya kulinda usalama wa watu au wafanyakazi na mitambo ya kuchakata kusafirisha na usambazaji gesi asilia .
Akizungumza wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi Duniani yanayofanyika Kitaifa mkoani Singida, Afisa Usalama na Mazingira Mahala Pa Kazi wa GASCO Bw. Mlotwa Simbeye amesema kuwa shughuli za gesi asilia zinahitaji umakini mkubwa wa usalama na ndio maana wanatumia mifumo ya kisasa ya utambuzi na ung’amuzi wa vihatarishi mbalimbali kama vile gesi kuvuja au majanga ya moto ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea.
Akiongea katika maonesho hayo, Mhandisi Hassan Temba amesema GASCO ina jukumu kubwa la usimamizi, uendeshaji na matenegezo ya mitambo ya Uchakataji, Usafirishaji na Usambazaji Gesi Asilia hapa nchini.
Pia, inahusika na ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia ikiwemo ujenzi wa bomba la usambazaji wa gesi kwa wateja wa viwandani na majumbani pamoja na ujenzi wa vituo vya mafuta na gesi asilia kwenye magari (CNG)
“Ndio maana tumeamua kushiriki maonesho haya ili Watanzania waweze kujua kazi za GASCO kwa maendeleo ya nchi,” amesema Temba.
Aidha, Afisa Maendeleo ya jamii wa TPDC Bw.Oscar Mwakasege amesema kuwa TPDC ina majukumu mbalimbali ikiwemo kusimamia miradi ya kimkakati ya utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini ukiwemo mradi wa utafiti wa mafuta Kitalu cha Eyasi Wembere ambao unagusa mikoa mitano (5) ikiwemo mkoa wa Singida (Wilaya ya Iramba na Mkalama).
‘‘Vilevile, TPDC ni mdau mkubwa wa maendeleo ya jamii kwani kupitia programu ya CSR miradi mbalimbali imetekelezwa ili kuleta ustawi wa na kudumisha mahusiano na jamii zinazopitiwa na miradi ya gesi asilia nchini. Mkoani Mtwara TPDC imekamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha Msimbati mkoani Mtwara’’. Amesema Oscar
Kauli mbiu ya maonesho hayo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ni ‘Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi’ ambapo mashirika na makampuni mbalimbali yameshiriki na kuonyesha mifumo yao ya afya na usalama kazini.