Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian, ameipongeza Halmashauri ya Mji Handeni kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo pamoja na kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 108 hadi kufikia Juni 7, 2025.
Akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kujadili hoja za ukaguzi, Dk Batilda ameeleza kuwa Halmashauri hiyo imekusanya Shilingi bilioni 2.439 ambapo Shs milioni 103 kimeelekezwa kwenye huduma ya lishe na Shs milioni 666.683 kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, ameeleza kuridhishwa na matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki ya manunuzi kama vile NEST, ambayo imesaidia kupunguza hoja za ukaguzi wa fedha.
Katika kikao hicho, Dk Batilda ameagiza menejimenti ya Halmashauri chini ya Mkurugenzi wake kuhakikisha kuwa hoja zote za ukaguzi zilizowasilishwa zinatekelezwa kikamilifu ifikapo Juni 30, 2025.
