Hisa za kampuni za Marekani na dola ya nchi hiyo vimeshuka thamani huku Rais Donald Trump akizidisha mashambulizi kwa bosi wa benki kuu ya Marekani kwa kutopunguza viwango vya riba.
Katika chapisho kupitia mtandao wa kijamii, Trump ametoa wito kwa mwenyekiti wa Hifadhi ya Shirikisho, Jerome Powell kupunguza viwango vya riba ili kusaidia kukuza uchumi.
"Uchumi unaweza kudorora, isipokuwa Bwana Mcheleweshaji, mpotofu mkuu, apunguze viwango vya riba sasa" aliandika Rais Trump.
Ukosoaji wa Trump juu ya jinsi Powell anavyoshughulikia uchumi wa Marekani unakuja wakati mipango yake mwenyewe ya ushuru imesababisha kushuka thamani kwa soko la hisa na kuibua hofu ya kuzorota kwa uchumi.
Mzozo wa rais huyo na Powell umeongeza msukosuko wa soko ambapo S&P 500, ambayo inafuatilia kampuni 500 kubwa zaidi za Marekani, ilishuka kwa takriban 2.4% siku ya Jumatatu na kupoteza takriban 12% ya thamani yake tangu kuanza kwa mwaka.
Kampuni ya Dow Jones Industrial Average imeshuka kwa 2.5% na imeshuka karibu 10% hadi sasa mwaka huu, huku Nasdaq imeshuka zaidi ya 2.5% na iko chini ya 18% tangu Januari.
Fahirisi ya dola ambayo hupima nguvu ya dola dhidi ya sarafu nyingine kama Euro pia imeshuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu mwaka 2022 huku viwango vya riba kwa deni la serikali ya Marekani pia vimepanda.
Ukosoaji wa Trump kwa Powell ulianzia muhula wake wa kwanza madarakani, iliripotiwa kwamba Trump alijadili juu ya kumfukuza kazi. Tangu kushinda uchaguzi huo, Powell amemtaka kupunguza gharama za kukopa.
Ukosoaji wa hivi punde unafuatia maonyo ya Powell kwamba ushuru wa Trump unaweza kupandisha bei ya bidhaa na kupunguza ukuaji wa uchumi.
Mnamo mwaka 2024 aliwaambia waandishi wa habari kuwa haamini kuwa Rais ana mamlaka ya kisheria ya kumwondoa madarakani.