Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura amefanya uhamisho wa makamanda watatu akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi.
Taarifa ya uhamisho huo imetolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ikiwa ni siku 302 tangu Katabazi alipoteuliwa rasmi kukalia kiti hicho, Agosti 19 mwaka jana.
Katabazi anatolewa kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma na kupelekwa ofisi ya makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Dodoma.
Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Galus Hyera ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli.
Mbali na kuhamishwa kwa Katabazi, pia Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Matride Kuyeto amehamishwa kutoka kuwa mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli.
“Uhamisho huo ni mabadiliko ya kawaida yanayofanyika ndani ya Jeshi la Polisi katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
