Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa vigezo sita vya kuzingatiwa na taasisi za kiraia zinazotarajia kutoa elimu ya mpiga kura na uraia kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
INEC pia ilizitaka taasisi zinazotaka kutoa elimu ya mpiga kura na uraia kutuma maombi yao kuanzia jana Aprili 21, 2025 hadi Mei 20, 2025 ambapo taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima ya Aprili 19, 2025 iliyotolewa jana ilieleza kuwa mwaliko huo umetolewa kwa kuzingatia kufungu cha 10 (1) (g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Namba 2 ya 2024.
“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake cha Aprili 3, 2025 imetoa mwaliko kwa taasisi na asasi za kiraia zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi wakati wa uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani 2025,” alisema.
INEC ilibainisha vigezo hivyo ni taasisi na asasi kusajiliwa na sheria za Tanzania, taasisi na asasi hizo kufanya kazi kwa kipindi kisichopungua miezi sita tangu kusajiliwa kwake.
Pia, kwa taasisi zenye watendaji wa kimataifa, INEC ilisema ni lazima watendaji wawili wakuu kati ya watatu wawe raia wa Tanzania.
Tume ilieleza kuwa taasisi au asasi hizo hazipaswi kujihusisha na uchochezi au kuvuruga amani katika utendaji wake na zinatakiwa kuwa na uzoefu wa kutoa elimu ya mpigakura na iwe tayari kujigharamia katika kutoa Elimu ya Mpigakura.
Aidha, tume pia ilisema taasisi na asasi zitakazo tuma maombi ya uangalizi wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia masharti yaliyopo kwenye mwongozo wa uchaguzi mkuu.
Asasi za kiraia na taasisi hizo zinapaswa kuainisha anuani ya taasisi au asasi zao, mahali taasisi au asasi husika inapofanyia kazi, shughuli zinazofanywa na taasisi au asasi husika kwa mujibu wa hati ya usajili.
Aidha, zinapaswa kuainisha mahali taasisi hizo inatarajia kwenda kuangalia uchaguzi huo, idadi, majina, na taarifa binafsi za watendaji wa taasisi au asasi zitawatumia katika usimamizi na uangalizi.
Pia, taasisi na asasi za kiraia zinatakiwa kuwasilisha majina na namba za simu za viongozi wao.
Pia, asasi hizo zinatakiwa kuambatanisha nakala vivuli na nyaraka ya usajili wa taasisi au asasi husika na nakala kivuli ya Katiba ya taasisi au asasi husika.
Tume ilieleza maombi hayo yanapaswa kutumwa katika mfumo wa Kusajili Watazamaji, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari na ilisisitiza kuwa maombi yatakayotumwa kwa njia tofauti na mfumo ulioainishwa hayatafanyiwa kazi.