Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametahadharisha kuwa eneo la Mashariki ya Kati lipo katika njia panda kuhusu ahadi ya suluhisho la mataifa mawili katika mzozo kati ya Israel na mamlaka ya Palestina.
Guterres ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ahadi hiyo ya suluhisho la mataifa mawili iko hatarini kutoweka kabisa na kuongeza kuwa utashi wa kisiasa wa kufanikisha lengo hilo unaonekana kuwa mbali zaidi sasa kuliko wakati wowote ule.
"Muda unakwenda suluhisho la mataifa mawili liko karibu kufikia hatua isiyoweza kurudi nyuma Jamii ya kimataifa ina jukumu la kuzuia ukaliaji wa kudumu na vurugu." amasema Guterres
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza mataifa kuchukua hatua zaidi na si kutoa kauli pekee na kueleza hatua mahususi za kufufua suluhisho la mataifa hayo mawili.
Amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika ukanda wa Gaza ambapo takribani Wapalestina 2,000 wameuawa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Machi yaliposambaratika.