Mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda yametia saini makubaliano ya awali ya amani yaliyohusisha ahadi ya kuandaa rasimu ya mkataba wa amani ifikapo Mei 2, 2025.
Huu ni mchakato muhimu wa kidiplomasia unaoendelea kuleta matumaini ya kumaliza vurugu zinazozikumba nchi hizo, hususani katika maeneo ya mashariki ya Kongo.
Makubaliano hayo yalitiwa saini mjini Washington, Marekani, na yanahusisha ahadi ya pande zote mbili kuepuka kutoa msaada wa kijeshi kwa makundi ya waasi.
Mkataba huo umefungua njia ya mazungumzo ya uwekezaji mkubwa wa umma na binafsi kutoka Marekani kwa nchi hizo mbili, hasa katika sekta ya madini ambapo Kongo inajivunia rasilimali kama vile tantalum, dhahabu, shaba, kobati, na lithiamu ambazo ni muhimu katika utengenezaji wa simu za mkononi na magari ya umeme.
Kwa upande mwingine, kundi linaloungwa mkono na Rwanda la M23, linajulikana kwa operesheni zake kubwa za kijeshi katika maeneo ya mashariki ya Congo. Hali hii imeongeza wasiwasi kuhusu usalama na amani katika eneo hilo.
Katika makubaliano hayo, pande hizo mbili pia zimekubaliana kuanzisha mfumo wa ushirikiano wa kiusalama ili kukabiliana na makundi ya waasi na vikundi vya kihalifu vinavyohatarisha amani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner, alieleza matumaini yake kwamba wananchi wa Kongo, hasa walioko mashariki mwa nchi, wanatarajia matokeo zaidi kuliko ahadi tu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alisisitiza kuwa makubaliano hayo ni fursa ya kujenga mkataba wa amani wa kudumu, akiongeza kwamba wanajadili namna ya kujenga minyororo mipya ya uchumi wa kanda hiyo na kuhusisha uwekezaji kutoka sekta binafsi ya Marekani.
Wakati huo, Marekani inazungumzia uwekezaji wa mamilioni ya dola kwenye madini ya Kongo, jambo ambalo linatarajiwa kuleta fursa za kiuchumi na ustawi katika kanda hiyo ya Maziwa Makuu.
Rubio, ambaye ni Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, alikiri kuwa amani ya kudumu katika Kanda ya Maziwa Makuu itafungua milango kwa uwekezaji mkubwa wa Marekani na mataifa mengine ya Magharibi, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa Congo na Rwanda.