Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua Mahabusu ya watoto Mkoani Mtwara na kueleza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya sita ni kulinda haki za watoto na kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini.
Mahabusu hiyo imezinduliwa Aprili 12, 2025 mkoani humo ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani inayofanyika Mkoani humo.
Dkt. Gwajima amesema mahabusu hiyo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuhakikisha watoto waliokinzana na sheria hawachanganywi na watu wazima magerezani hali inayokiuka Sheria ya Mtoto Sura ya 13 huku akieleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Kuboresha Haki Jinai, ikiwemo kuanzisha mahabusu na Shule za Maadilisho katika mikoa mbalimbali ili kuweka mazingira bora kwa watoto wanaoshtakiwa ambapo hadi sasa, mikoa 16 tayari imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa mahabusu hizo.
Amesisitiza kuwa Mahabusu ya Mtwara itatumika kuwahifadhi watoto pindi wanapokinzana na sheria, badala ya kuwaweka gerezani na watu wazima, hatua itakayosaidia kulinda haki na ustawi wa mtoto. Pia, ametoa pongezi kwa viongozi wa Wizara za kisekata na Taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wote kwa ushirikiano wao kufanikisha uwepo wa huduma hiyo muhimu.
Aidha, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Mahakama, Jeshi la Polisi, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha watoto wanachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, hususani kuzingatia uhalisia wa umri wao na kuwasilisha taarifa sahihi kwa ajili ya uamuzi sahihi wa kimahakama.