Safari ya kiongozi wa kihafidhina wa Ujerumani, Friedrich Merz, kuwa kansela mpya wa Ujerumani imeingia walakini asubuhi ya leo baada ya kushindwa kupata kura za kutosha kwenye duru ya mwanzo ya upigaji kura bungeni.
Katika hatua ambayo haikutarajiwa Merz anayeongoza chama cha CDU alishindwa kupata wingi wa kutosha bungeni wakati kura ilipopigwa leo ambapo alikuwa ametazamiwa na wengi kwamba angelipita kwenye kura ya moja kwa moja, lakini alikosa kura sita kati ya kura 316 alizokuwa anazihitajia.
Waliompigia kura ya ndio walikuwa wabunge 310 kati ya 630 waliomo bungeni.
Vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni vilipaswa kujipanga upya, na kupiga kura mpya ndani ya siku 14 ya ama kumchaguwa tena Merz ama mgombea mwengine atakayewekwa kwa kura ya moja kwa moja.
Muungano wa vyama viwili vya kihafidhina vya CDU-CSU unaoongozwa na Merz ulishinda uchaguzi mkuu wa mwezi Februari, lakini kwa kupata asilimia 28.5 tu ya kura, matokeo yaliyoulazimisha kuwa na mshirika angalau mmoja kuweza kuunda serikali.
Merz aliyekuwa anatazamiwa kutangazwa kuwa kansela wa 10 wa Ujerumani tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, alikuwa amekubaliana kuunda Serikali ya mseto na chama cha siasa za mrengo wa kati kushoto, SPD, ambacho kilipata asilimia 16.4 tu ya kura, yakiwa matokeo mabaya kabisa kwa chama hicho
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, ambacho ndicho kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Februari kuwa kupata takribani asilimia 21, kiliyafurahikia matokeo hayo yaliyomuangusha Merz, kikisema kiongozi huyo amelipwa kwa makosa yake ya kisiasa.