Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limesema uwezekano wa migogoro ya kibiashara, madai ya kimkataba na mingine iliyopo na inayojitokeza kwenye sekta mbalimbali nchini, ikiwemo ya ujenzi, inawezekana bila wahusika wa migogoro hiyo kupelekana mahakamani.
Akizingumza Dar es Salaam hivi karibuni wakati mafunzo hayo yaliyoandaliwa na NCC, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Dk Fauz Twaib ambaye ni miongoni mwa wafundisha njia hizo, alisema kinachotakiwa ni wasuluhishi kuzingatia maadili, sheria na taratibu za usuluhishi.
Alisema njia zaidi ya nne za kusuluhisha migogoro mbali na kushitakiana mahakamani, zinafundishwa na kuwawezesha waliopata mafunzo hayo kuamua kwa weledi ipi inafaa kulingana na mazingira na hali halisi ya mgogoro husika.
Kwa mujibu wa Dkt Twaib, kwa kutumia njia hizo mbadala, hakuna upande unaojeruhiwa kwa sababu pande zote zinahusika katika hatua zote muhimu za usuluhishi, ikiwemo kuchagua nani ahusike kuwasuluhisha.
"Ikiwa hakuna mazingira yoyote ya tamaa inayoweza kusababisha upendeleo, mfano rushwa au chochote kile kitakachofanya usuluhishi uegemee upande mmoja, mlolongo wa kisuluhishi hautokei hivyo kuokoa muda na gharama" anasema Dkt Twaibu.
Kwa upande wake, Mhandisi wa kujitegemea, Julius Mamiro anayefundisha mbinu hizo, hususani majadiliano ya kisuluhishi ya madai ya kimkataba ya ujenzi alisema, maadili mazuri yanafanikisha usuluhishi.
alieleza kuwa jambo kubwa wanalolisisitiza ni wataalam wa masuala yote yanayoweza kuhusika kwenye migogoro iwe ya sekta ya ujenzi au ya kibiashara nje ya sekta ya ujenzi au ya kimkataba kwenye sekta yoyote wawe na elimu ya namna ya kuitatua migogoro yao bila kupelekana mahakamani kisha watekeleze mbinu walizofundishwa kwa kuzingatia maadili.