Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesifiwa nyumbani kwa jinsi alivyosimama kwa utulivu na staha mbele ya tuhuma nzito na zisizo na msingi alizorushiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Katika moja ya matukio yaliyozua taharuki, Trump alimwonyesha Ramaphosa video yenye madai ya "mauaji ya halaiki dhidi ya wakulima wazungu" nchini Afrika Kusini madai ambayo yamekanushwa mara kwa mara na Pretoria na ambayo wataalamu wameyaeleza kuwa ya kupotosha.
Lakini licha ya mtego huo wa kisiasa, Ramaphosa alijibu kwa utulivu, na hata kumzawadia Trump kitabu kuhusu mchezo wa gofu.
Watetezi wa haki za binadamu na raia wa kawaida walitoa kauli za kuunga mkono mtindo wa Ramaphosa.
Wengine walitaka majibu makali zaidi dhidi ya uongo huo, lakini wengi waliona uongozi wake kama kielelezo cha diplomasia ya kweli “Nadhani nchi yetu imejieleza vyema na kuweka ukweli mezani,” alisema mwanaharakati Ulrich Steenkamp.
Kwa upande wa matokeo ya kisiasa, Ramaphosa alisema mkutano wao umefungua mlango kwa mazungumzo ya kina kuhusu biashara na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Marekani ni mshirika wa pili kwa ukubwa wa kibiashara kwa Afrika Kusini baada ya China, na hatua ya Marekani kuashiria kuanza tena majadiliano ya biashara ilipokelewa kama mafanikio makubwa kwa Ramaphosa.