Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanzisha mpango maalum wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kidato cha sita waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi, ili kujiunga na shahada ya kwanza katika vyuo vikuu vinavyoongoza duniani.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni mjini Dodoma, Profesa Mkenda amesema mpango huo unaoitwa Mama Samia 360 – DSP/AI+ utahusisha taaluma za sayansi ya takwimu, akili bandia na kompyuta.
Prof. Mkenda amesema utekelezaji wa mpango huu umegawanywa katika hatua tatu ikiwemo kambi ya maandalizi ya miezi 10 kwa wahitimu wa kidato cha sita, kuwatafutia nafasi za udahili na ufadhili vyuo vya nje na kuwaendeleza wenye shahada ya kwanza katika Taasisi ya Nelson Mandela na taasisi ya India, kampasi ya Zanzibar.
Aidha, alisema serikali itaendelea kufadhili wanafunzi wa fani ya sayansi ya nyuklia na kuwekeza kwenye tafiti, ambapo miradi 130 itaendelezwa na mingine 155 kuanzishwa katika sekta za afya, elimu, kilimo, biashara na mazingira.
Wizara hiyo imeomba Shilingi Trilioni 2.436, ambapo zaidi ya Bilioni 688 ni kwa matumizi ya kawaida na Shilingi Trilioni 1.747 kwa miradi ya maendeleo.
