Serikali ya Tanzania imesema imeliona azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya May 08,2025 kuhusu kesi za kisheria zinazoendelea nchini lakini haijaridhishwa na hatua hiyo kwakuwa Bunge hilo limetoa maamuzi kwa kuzingatia taarifa za upande mmoja bila kushauriana kwanza kwa njia za kidiplomasia na Tanzania huku ikisisitiza kwamba Serikali haiwezi kuingilia Mhimili wa Mahakama.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema “Ingawa Tanzania inaheshimu uhuru wa kitaasisi wa Bunge la Ulaya na inathamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya bado inaona kuna umuhimu wa kufafanua baadhi ya mambo na kusisitiza wake wa muda mrefu kwenye maadili ya kidemokrasia, utawala bora, na utawala wa sheria”
“Tangu March 2021, Tanzania imefanya mageuzi ya kisiasa na kisheria chini ya falsafa ya 4Rs ambayo imezaa matokeo ya thabiti ikiwemo kurejesha uhuru wa kisiasa, upanuzi wa haki za raia, kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, na kupitishwa kwa sheria mpya za uchaguzi March 2024, ambazo zilisababisha kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi”
“Tanzania ni nchi huru yenye katiba yake na inatawaliwa na utawala wa sheria hivyo masuala ya kisheria yanashughulikiwa kwa uhuru na Mahakama kama moja ya Mhimili wa Dola kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ambapo Mhimili wa Serikali hauwezi kuingili kesi zinazoendelea Mahakamani, hivyo, kauli zinazohimiza Serikali iingilie utendaji katika kesi zinazoendelea za Mahakama sio tu hazifai lakini pia zinapingana na kanuni za msingi za uhuru wa Mahakama kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania”
“Tanzania ina wasiwasi na mwelekeo unaoendelea kama ulivyoonekana katika azimio la Bunge la Ulaya la baadhi ya Wadau wa kimataifa kutoa hukumu kwa kuzingatia taarifa zisizotosha au za upande mmoja, bila kushauriana kwanza kupitia njia za kidiplomasia, kesi za kisheria nchini zinachukuliwa kwa uchunguzi wa kipekee, pia maendeleo yaliyopatikana katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari, ushirikishwaji wa kisiasa, mageuzi ya uchaguzi, na ujenzi wa amani wa kikanda hayajazingatiwa kwenye maoni ya Bunge la Ulaya”
