Serikali ya Tanzania imesisitiza msimamo wake wa kudumisha amani, kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu 2025 unakuwa huru na wa haki na kulinda haki za msingi na uhuru wa Raia wote kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Hayo yamesemwa kwenye taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyolenga kutoa ufafanuzi kuhusu maazimio yaliyopitishwa na Bunge la Ulaya May 08,2025 kuhusu kesi za kisheria zinazoendelea nchini “Huku Tanzania ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, Serikali inasisitiza tena msimamo wake usioyumba kwa kudumisha amani, kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, na kulinda haki za msingi na uhuru wa Raia wote kwa mujibu wa Katiba yake”
“Tanzania itaendelea kuweka nguvu kusimamia haki na heshima ya Watu wote kwa usawa kama Katiba inavyosema lakini ni muhimu kutoa ufafanuzi kwamba masuala yanayohusiana na mwelekeo wa kujamiiana yanashughulikiwa wazi ndani ya mfumo wa Katiba ya Tanzania, sheria za kitaifa, maadili ya kitamaduni, na kanuni za jamii, Tanzania inasisitiza tena kwamba ushirikiano wowote lazima uwe wa msingi wa kuheshimiana maadili, ikiwa ni pamoja na heshima kwa uhuru wa nchi, katiba, mifumo ya kisheria, na utambulisho, huku ushirikiano wa siku zijazo ukilenga vipaumbele vya pamoja katika maendeleo, utawala bora, ukuaji wa uchumi, ustawi wa Watu, na hali ya msingi ya maisha”
“ Tanzania inaendelea kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya na iko tayari kwa mazungumzo ya wazi, ya heshima na yanayotegemea ushahidi kuhusu masuala ya pamoja lakini mazungumzo haya lazima yawe ya msingi wa uwazi, haki, heshima ya pande zote, na uthamini kamili wa uhuru wa Taasisi za kila nchi, katiba, pamoja na muktadha wa kisheria na kitamaduni”
“Tanzania inakaribisha msaada unaoendelea kutoka Umoja wa Ulaya na Washirika wote wa kimataifa wanaojihusisha kwa nia njema na uelewa wa usawa wa wazi wa safari ya kidemokrasia ya nchi yetu na iko tayari kushirikiana na kuwapa uelewa zaidi wale ambao bado hawajafahamu maadili ya kitamaduni ya Tanzania”
