Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na utalii endelevu, sambamba na mabadiliko ya kiuchumi kutoka nchi ya kipato cha chini hadi kipato cha kati cha juu.
Mkakati huo unalenga kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya jamii na kuongeza mapato ya Taifa kupitia matumizi bora ya rasilimali za asili.
Akizungumza katika warsha ya kitaifa inayoangazia Uhifadhi na Mchango wake katika Utalii na Maendeleo ya Jamii, iliyofanyika jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana alisema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea misaada na ruzuku, bali inapaswa kuwa mshirika wa maendeleo kupitia sekta ya utalii.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na utalii unaonufaisha wananchi moja kwa moja.
Dk. Chana alibainisha kuwa licha ya mafanikio ya ongezeko la idadi ya watalii kutoka milioni 1.7 mwaka 2021 hadi milioni 5.3 mwaka 2024, na mapato kutoka dola bilioni 1.3 hadi bilioni 3.9, bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza manufaa kwa jamii. Alitoa wito kwa wataalamu na wadau kuendeleza tafiti na ubunifu katika sekta hiyo.
Warsha hiyo, iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, inalenga kujadili mbinu bora za kuendeleza utalii unaohimiza uhifadhi wa mazingira, kukuza ajira, na kuboresha maisha ya Watanzania kupitia utalii jumuishi na wa kisasa.