Serikali imependekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa viwango vipya kwenye bidhaa za soseji na ice cream, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza mapato, kulinda afya za wananchi na kuimarisha viwanda vya ndani.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Juni 12 2025, bungeni jijini Dodoma, ice cream zinazozalishwa nchini zitatozwa ushuru wa asilimia 5, huku zinazoagizwa kutoka nje zikitozwa asilimia 10. Bidhaa hizi zimetambulika kwa HS Code 2105.00.00, na hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa zaidi ya Sh milioni 119,465.5.
Aidha, soseji na bidhaa zinazofanana zinazozalishwa ndani zitatozwa ushuru wa asilimia 5, na asilimia 10 kwa zile kutoka nje ya nchi, chini ya HS Code 1601.00.00. Serikali inatarajia kupata mapato ya takribani Sh milioni 2,413.9 kutokana na kodi hiyo.
Dk. Mwigulu amesema hatua hizi pia zinalenga kuvutia uwekezaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, sambamba na kuchochea uzalishaji wa ndani kwa bidhaa zinazotengenezwa kwa malighafi ya hapa nchini.
