Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, ametembelea Makao Makuu ya Wakala wa Nishati Jadidifu wa Falme ya Morocco (MASEN) na kufanya mazungumzo na uongozi wa taasisi hiyo, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Tariki Ameziane Moufaddal.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco katika sekta ya nishati, hasa uzalishaji wa umeme na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Pande hizo mbili zimekubaliana kuteua wataalamu kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ili kuhakikisha manufaa kwa nchi zote mbili.
Bw. Moufaddal ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuimarisha miundombinu ya uzalishaji wa nishati. "Tanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika katika juhudi za kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa wananchi wote," amesema.
Londo aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Ali Mwadini, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, REA, TPDC na Wizara ya Mambo ya Nje. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kukuza ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu za maendeleo.
