VIRUSI vya West Nile vimebainika kwa mara ya kwanza nchini Uingereza na vinahusishwa na mbu, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Usalama la Afya la Uingereza (UKHSA).
Hata hivyo, shirika hilo limewahakikishia wananchi kuwa hatari ya kuambukizwa kwa sasa ni ndogo, huku likitoa wito wa kuchukua tahadhari.
Kwa mujibu wa UKHSA, virusi hivyo vinaweza kusababisha maradhi makali kwa binadamu, hasa ikichangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini hadi sasa hakuna ushahidi wa kuenea kwa virusi hivyo kati ya mbu ndani ya Uingereza.
Kwa kawaida, virusi hivyo huenezwa na mbu wanaouma ndege na vimekuwa vikigundulika katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo barani Ulaya.
Tangu mwaka 2000, hakuna kisa chochote cha maambukizi ya binadamu kilichothibitishwa nchini humo, isipokuwa visa saba vilivyogundulika kwa wasafiri waliotoka katika nchi zilizoathirika.
Kwa sasa, virusi vya West Nile vimeenea katika maeneo mbalimbali ya Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na Ulaya, huku ongezeko la maambukizi likishuhudiwa katika miaka ya karibuni.
