Amri ya kutotoka nje usiku imetangazwa huko Los Angeles nchini Marekani huku maafisa wa mji huo wakipambana kuyadhibiti maandamano ambayo Rais Donald Trump alidai kuwa ni uvamizi unaofanywa na adui wa kigeni.
Matukio ya uporaji na uharibifu yamekikumba kitovu cha jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini Marekani huku maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani kuhusu kukamatwa kwa wahamiaji yakigeuka kuwa vurugu nyakati za usiku ambapo Meya Karen Bass amewaambia waandishi habari kuwa amechukua hatua hiyo ili kuzuia uharibifu na uporaji.
Mitaa ya katikati ya mji wa Los Angeles itafungwa kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi huku jeshi la Polisi likimesema zaidi ya watu 500 wamekamatwa tangu maandamano yalipoanza mwishoni mwa wiki.
Maandamano pia yameshuhudiwa katika miji mingine ya Marekani ikiwemo New York, Atlanta, Chicago na San Francisco.
Trump ameamuru askari 4,000 wa Ulinzi wa Taifa kwenda Los Angeles, pamoja na wanajeshi 700 wa kitengo maalum, katika kile amedai ni hatua ya lazima ya kuchukua udhibiti licha ya polisi wa eneo hilo kusisitiza kwamba wanaweza kushughulikia hali hiyo.