Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka za kuvunja nyumba iliyojengwa kimakosa katika kiwanja namba 1/31 kilichopo Block D, Iyumbu North jijini humo.
Waziri Ndejembi ametoa agizo hilo alipotembelea eneo hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa msimamizi wa mirathi wa familia ya marehemu Thobias Msigwa ambaye ni mmliki halali wa viwanja namba 1/30, 1/31, 1/32 na 1/33 kitalu D, Iyumbu North.
Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa mwenye hati halali ya kiwanja hicho ni msimamizi wa mirathi ya marehemu Thobias Simon Msigwa ambaye ni mke wake Prisca Lulambo.
Aidha, Waziri Ndejembi ametoa rai kwa watu kuacha kuvamia maeneo ya watu wengine ambayo yana umiliki halali na nyaraka halali katika Jiji la Dodoma na maeneo mengine nchini.
