Rais Donald Trump ametangaza kusitisha kwa siku 90 nyongeza ya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka mataifa mengine huku akikosa kuilegezea China.
Katika mabadiliko makubwa ya sera, saa chache baada ya ushuru dhidi ya takriban washirika 60 wa biashara wa Marekani kuanza, Trump alisema alikuwa akiidhinisha "kupunguzwa kwa ushuru wa asilimia 10%" wakati mazungumzo yakiendelea.
Hata hivyo aliongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka China hadi asilimia 125%, akiishutumu Beijing kwa "ukosefu wa heshima" baada ya kulipiza kisasi kwa kusema kuwa ingetoza ushuru wa 84% kwa bidhaa za Marekani.
"Itafika wakati China igundue kuwa siku za kuvuna kutoka kwa Marekani na nchi zingine sio endelevu au kukubalika," anasema Trump.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisisitiza kuwa mabadiliko ya sera hayajaathiriwa na anguko la kimataifa la kiuchumi, lakini mwandamizi wa chama cha Democrat Chuck Schumer alisema uamuzi huo unaonyesha Trump anayumba na kurudi nyuma.
Akihojiwa na waandishi wa habari kuhusu athari za kujibizana na China kibiashara, Trump amesema anaamini watafikia makubaliano na kiongozi wa China.
"Nadhani Rais Xi ni mtu anayefahamu fika anachokifanya.Ni mwerevu,anaipenda nchi yake,hilo nafahamu vyema,namjua vizuri na nadhani atataka kufikia makubaliano,nadhani hilo litafanyika.Tutapata simu wakati fulani na kutaafikiana,litakuwa jambo jema kwa na kwetu na litakuwa jambo jema kwa ulimwengu na ubinadamu", ameongeza Trump.
Hata hivyo, uamuzi huu mpya wa Trump haujaathiri tangazo la awali la ushuru ambao unaendelea kutekelezwa tangu tarehe 2 mwezi Aprili ikiwa ni ni pamoja na asilimia 25% ya ushuru wa kuagiza kwa magari na vipuri vya magari vinavyoingia Marekani, na ushuru zaidi wa 25% kwa bidhaa zote za chuma na alumini.
Ushuru wa kimataifa wa Trump umesababisha msukosuko mkubwa zaidi wa biashara ambao hujawahi kutokea katika miongo kadhaa.