Tume Maalum umeundwa katika bunge la Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo, kuanza kujadili suala la kuondolewa kwa kinga ya kutokamatwa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.
Tume hiyo ina masaa 72 kuwasilisha ripoti yake kwa bunge la Seneta.
Mjadala huo uliofanyika wakati wa kipindi cha kikao maalum jana, Alhamisi.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa na mgawanyiko bungeni wengine wakiunga mkono hoja hiyo ilihali wengine wakirejelea kifungu cha 224 cha sheria za utaratibu wa Seneti, wakiamini kwamba utaratibu huu unapaswa kuwasilishwa kwa kupigiwa kura bungeni.
Ikiwa hoja ya kutaka aondolewe kinga itaungwa mkono, atapoteza hadhi yake ya kuwa seneta wa kudumu na hivyo basi kuweza kushtakiwa.
Kabila anashukiwa kuwa na uhusiano na Congo River Alliance, muungano wa makundi ya waasi.
Anashtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na kushiriki katika harakati za uchochezi.
Vitendo hivyo vinadaiwa kutokea baada ya muda wake wa urais.
Wabunge wa Uganda wameidhinisha bajeti inayopendekezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki itatumia shilingi trilioni 72.4 za Uganda (dola bilioni 20) katika mwaka wa fedha wa 2025/26 (Julai-Juni), ikiwa ni mabadiliko kidogo kutoka kwa matumizi ya mwaka unaoishia mwezi ujao ambayo yanafikia shilingi trilioni 72.1, bunge lilisema kwenye ujumbe wa mtandao wa kijamii wa X Mei 15, 2025.
"Bunge limezingatia na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka ya fedha 2025/2026," ilisema.
Bunge halikusema ni sekta zipi zitapokea fedha nyingi lakini serikali iliwahi kusema siku za nyuma, vipaumbele vya matumizi katika mwaka ujao wa fedha vitakuwa katika sekta ya kilimo, utalii na madini yakiwemo mafuta ya petroli.
Waziri wa Fedha Matia Kasaija anatazamiwa kuwasilisha bajeti hiyo bungeni rasmi Juni 12 na kutoa maelezo zaidi kuhusu mahali pesa hizo zitatumika.
Uganda inatekeleza miradi ya miundombinu ili kuanza uzalishaji wa kibiashara wa mafuta ghafi mwaka ujao.
Miundombinu hiyo inajumuisha bomba la mafuta ghafi lenye thamani ya dola bilioni 5 kusaidia nchi hiyo isiyo na bandari kusafirisha mafuta yake kwenye masoko ya kimataifa kupitia Tanzania.