Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuongeza ubunifu kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa katika kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kupitia shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini sambamba na utoaji wa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Mhandisi Samamba ametoa kauli hiyo leo Mei 13, 2025 kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa makamishna wapya wa Tume ya Madini jijini Dodoma yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu Sekta ya Madini sambamba na majukumu ya Tume ya Madini.
Makamishna wapya walioteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan ni Mhandisi Theonestina Mwasha na Dk. Theresia Numbi.
Samamba amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini Aprili 2018 ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini umeongezeka na kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuwataka Makamishna wapya kuendelea kubuni mikakati mipya ya kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki kwenye shughuli za madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.
“Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana hususan ushiriki mkubwa wa watanzania kwenye Sekta ya Madini na kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, ninawataka kuongeza ubunifu hasa kwenye usimamizi wa eneo la utoaji wa leseni za madini, ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR) ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uendelee kukua.” Amesema.
Akielezea mafanikio katika Sekta ya Madini kwa kifupi, Mhandisi Samamba amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa 30, Maafisa Migodi Wakazi 13, Masoko ya Madini 43 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 109.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk. Janet Lekashingo amewapongeza makamishna wapya kwa uteuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuahidi ushirikiano kutoka kwa watendaji na watumishi wa Tume ya Madini.


Bunge limepitisha kwa kishindo jumla ya Sh Trilioni 2.439 bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuwezesha utekelezaji wa malengo ya wizara na taasisi zake yaliyoanishwa kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Bajeti hiyo imepitishwa kwa asilimia 100 leo Mei 13 ikiwa na mchanganuo wa Sh bilioni 688.6 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Sh bilioni 635.2 ni kwa ajili ya mishahara na Sh bilioni 53.3 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Utekelezaji wa bajeti hiyo utajikita zaidi katika maeneo matano ya vipaumbele ambayo ni i) kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya sheria, Uandaaji wa miongozo, na utoaji wa mafunzo, ii) Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya Amali katika shule za sekondari na vyuo vya Amali, iii) Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya Amali, Msingi, Sekondari na Ualimu, iv) Kuongeza na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na v) Kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, Matumizi ya Sanyansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.
Wabunge wamempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda (Mb) kwa utulivu wa kiutendaji katika wizara yake na mshikamano alionao na watendaji wote wa Wizara na kumsihi kusimamia kwa weledi mkubwa wizara hiyo ambayo ni msingi wa maendeleo ya nchi.
Kati ya fedha zilizopitishwa, zaidi ya Sh trilioni 1.7 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Sh 1.186 ni fedha za ndani na Sh 560.8 ni fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO imeidhinishiwa jumla ya Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Mishahara ni Sh bilioni 1.5 na Matumizi Mengineyo ni Sh bilioni 1.7

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama Vya Ushirika (COASCO) limekabidhiwa magari matano ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Magari hayo ni kati ya 38 yaliyokabidhiwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwenye Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pamoja na mitambo ya uchimbaji visima, itakayotumika katika shughuli za wizara na Taasisi zake za umwagiliaji.
Akikabidhi magari hayo kwa shirika hilo, Waziri Bashe amesema wameanza kuisaidia COASCO ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
“Angalau tumeanza kuisaidia COASCO ili iweze kutimiza wajibu wake. Tunaamini utendaji wa COASCO kwani sasa hivi wana rasilimali za kibajeti wameanza kupata, vitendea kazi wameanza kupata ili waweze kutimiza wajibu na kuonesha thamani ya fedha na naamini maono ya COASCO yatabadilika.” Alisema Bashe.
Aidha, alisema wizara yake inatarajia kuanzisha mpango wa ruzuku ya uchimbaji visima kwa ajili ya wakulima wa kipato cha chini, ambapo visima vitachimbwa bila malipo.

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeridhishwa na juhudi zilizochukuliwa na Magereza Mkoa wa Tanga kwa kuanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia katika kuandaa chakula cha wafungwa wa zaidi ya 560 tofauti na hapo awali ambapo matumizi ya kuni na mkaa yalikuwa ni zaidi ya asilimia 100.
Akizungumza baada ya kutembelea Gereza la Maweni mkoani Tanga leo Mei 13, Balozi Radhia Msuya, amesema Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeridhishwa kwa kiwango kikubwa na hatua zilizochukuliwa Magereza mkoani humo katika kutekeleza agizo lililotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, mwaka mmoja uliopita kuwa taasisi zote zinazowahudumia watu zaidi ya 100 kuacha kutumia nishati chafu (kuni na mkaa) ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira.
Baada ya kutembelea na kujionea miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia katika gereza hilo, Wajumbe wa Bodi REB, Wakili Mwantum Sultan na James Mabula, wamesema wameridhishwa kwa hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo na kuongeza kuwa juhudi hizo, zitasaidia kufikia lengo la agizo la Rais Samia ambapo Magereza Tanzania Bara yatapata Sh bilioni 35 kama ruzuku kutoka serikalini kupitia REA ili kutekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati Safi ya Kupikia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Tanga, ACP, Fredrick Massawe amesema magereza imejiwekea malengo endelevu ya matumizi ya Nishati Safi huku akishukuru ushirikiano uliopo baina yao na REA ambao utawezesha Magereza kupata majiko banifu, mitungi ya gesi ya LPG, upatikanikanaji wa mkaa banifu (Rafiki Briquettes) pamoja na ununuzi wa mashine 61 za kutengeneza mkaa mbadala pamoja na kukuza uwezo kwa Watumishi 280 wa Magereza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Naye Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi ya Nishati Safi, Mhandisi, Emmanuel Yesaya kutoka REA amesema, tarehe 13 Septemba mwaka jana REA ilisaini mkataba na Magereza ambapo Serikali itatoa ruzuku kwa ajili ya kuwezesha uboreshaji wa miundombinu ya Nishati Safi ya kupikia kwa Magereza yote Tanzania Bara ambapo utekelezaji ukaanza mwezi Desemba, 2025 na uda wa utekelezaji wa mradi huo utakuwa miezi 36 huku gharama ya mradi itakuwa Sh bilioni 35.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanzisha mpango maalum wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kidato cha sita waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi, ili kujiunga na shahada ya kwanza katika vyuo vikuu vinavyoongoza duniani.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni mjini Dodoma, Profesa Mkenda amesema mpango huo unaoitwa Mama Samia 360 – DSP/AI+ utahusisha taaluma za sayansi ya takwimu, akili bandia na kompyuta.
Prof. Mkenda amesema utekelezaji wa mpango huu umegawanywa katika hatua tatu ikiwemo kambi ya maandalizi ya miezi 10 kwa wahitimu wa kidato cha sita, kuwatafutia nafasi za udahili na ufadhili vyuo vya nje na kuwaendeleza wenye shahada ya kwanza katika Taasisi ya Nelson Mandela na taasisi ya India, kampasi ya Zanzibar.
Aidha, alisema serikali itaendelea kufadhili wanafunzi wa fani ya sayansi ya nyuklia na kuwekeza kwenye tafiti, ambapo miradi 130 itaendelezwa na mingine 155 kuanzishwa katika sekta za afya, elimu, kilimo, biashara na mazingira.
Wizara hiyo imeomba Shilingi Trilioni 2.436, ambapo zaidi ya Bilioni 688 ni kwa matumizi ya kawaida na Shilingi Trilioni 1.747 kwa miradi ya maendeleo.