Mahabusu ya Watoto yazinduliwa mkoani Mtwara  lengo likiwa ni kulinda haki na ustawi wa mtoto.

Mahabusu ya Watoto yazinduliwa mkoani Mtwara lengo likiwa ni kulinda haki na ustawi wa mtoto.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua Mahabusu ya watoto Mkoani Mtwara na kueleza kuwa  dhamira ya Serikali ya Awamu ya sita  ni kulinda haki za watoto na kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini.

Mahabusu  hiyo imezinduliwa Aprili 12, 2025 mkoani humo ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani inayofanyika Mkoani humo.

Dkt. Gwajima amesema mahabusu hiyo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuhakikisha watoto waliokinzana na sheria hawachanganywi na watu wazima magerezani hali inayokiuka Sheria ya Mtoto Sura ya 13 huku  akieleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Kuboresha Haki Jinai, ikiwemo kuanzisha mahabusu na Shule za Maadilisho katika mikoa mbalimbali ili kuweka mazingira bora kwa watoto wanaoshtakiwa ambapo hadi  sasa, mikoa 16 tayari imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa mahabusu hizo.

Amesisitiza kuwa Mahabusu ya Mtwara itatumika kuwahifadhi watoto pindi wanapokinzana na sheria, badala ya kuwaweka gerezani na watu wazima, hatua itakayosaidia kulinda haki na ustawi wa mtoto. Pia, ametoa pongezi kwa viongozi wa Wizara za kisekata na Taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wote kwa ushirikiano wao kufanikisha uwepo wa huduma hiyo muhimu.

Aidha, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Mahakama, Jeshi la Polisi, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha watoto wanachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, hususani kuzingatia uhalisia wa umri wao na kuwasilisha taarifa sahihi kwa ajili ya uamuzi sahihi wa kimahakama.

"Chama cha siasa ambacho hakitasaini kanuni za  maadili ya uchaguzi mkuu  hakitoruhusiwa kushiriki" - Ramadhani Kailima

"Chama cha siasa ambacho hakitasaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu hakitoruhusiwa kushiriki" - Ramadhani Kailima

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyama vya siasa na Serikali  Aprili 12, 2025 wanatarajia kusaini Kanuni za maadili ya uchaguzi zitakazotumika kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na vyombo vya habari mkoani Dodoma leo  Aprili 11, 2025 mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhan amesema chama cha siasa ambacho hakitasaini maadili hayo hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Ndugu. Kailima amesema maadili hayo yameandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ambacho kinaitaka Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.

Amesema kifungu hicho kinaelekeza kuwa kanuni za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na Tume na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.

Ameongeza kuwa tayari maandalizi yote muhimu yameshafanyika na mawasiliano yameshafanyika baina ya Tume, Serikali na vyama vya siasa na kwamba kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wahusika jijini Dodoma kwa ajili ya kusaini kanuni hizo za maadili kesho.

Amefafanua kuwa zoezi hilo litafanyika kwa siku moja tu na kwamba baada ya hapo chama ambacho hakijasaini kanuni hizo za maadili hakitapata fursa ya kusimamisha wagombea.

Katika hatua nyingine, Kailima amesema Tume inaendelea vizuri na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba tayari imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  huku  maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwa awamu ya pili yanaendelea ambapo Tume inatarajiwa kutangaza ratiba ya zoezi hilo hivi karibuni.

Kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, ambacho kinaipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili, kati ya uchaguzi mkuu mmoja uliomalizika na siku moja kabla ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mkuu unaofuatia.

Tayari Tume imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari ambao ulifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 hadi tarehe 25 Machi, 2025.

"Wiki ya Afya Inaweka Mikakati ya Pamoja ya Kuboresha Huduma za Afya Nchini" Dkt. Dugange

"Wiki ya Afya Inaweka Mikakati ya Pamoja ya Kuboresha Huduma za Afya Nchini" Dkt. Dugange

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, amesema wiki ya afya ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa ya kujikumbusha na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza katika kilele cha wiki hiyo jijini Dodoma Aprili 8, 2025 kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za uhakika, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake makubwa katika kuiinua sekta hiyo.

“Huduma za afya zinaendelea kuimarika kupitia uwekezaji kwenye vifaa tiba na miundombinu. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, zaidi ya shilingi trilioni moja zimetumika kuboresha huduma za afya katika ngazi ya msingi,” amesisitiza Dkt. Dugange.

Aidha, Naibu Waziri Dugange amewapongeza watumishi wa sekta ya afya kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na kuhimiza kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha huduma za afya zinafikia kila mtanzania kwa ubora unaotakiwa.

Dkt. Nchimbi Awaasa Waandishi wa Habari Kutumia Kalamu Zao Kuimarisha  Amani Katika Jamii.

Dkt. Nchimbi Awaasa Waandishi wa Habari Kutumia Kalamu Zao Kuimarisha Amani Katika Jamii.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi , Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari kuzitumia kalamu zao vizuri ili kuchochea amani, utulivu, na kuongeza umoja katika jamii, badala ya kuzusha vurugu.

Ametoa wito huo April 04,2025  mjini Songea, mkoani Ruvuma katika Mkutano mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuelekea uchaguzi wa viongozi wa jukwaa hilo, unaofanyika leo  Aprili 5, 2025, wenye lengo la kumpata  Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa jukwaa hilo.

Balozi Nchimbi amepongeza kazi kubwa zinazofanywa na wahariri katika kuzitangaza 4R za Rais Samia Suluhu Hassan, ambazo sasa jamii imeanza kuzielewa na kusema ni dhahiri kwamba wananchi wanatambua umuhimu wa vyombo vya habari. Ameiomba TEF kuendelea kufanya kazi ya kujenga jamii ya Tanzania.

Aidha, amewapongeza wahariri kwa kuwa chujio la habari zote katika Taifa, akieleza kuwa endapo wangetumia nafasi zao vibaya, jamii ingekuwa katika hali tofauti na ilivyo sasa.

Balozi Nchimbi alibainisha kuwa Chama cha Mapinduzi kinatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari na dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha vyombo hivyo vinafanya kazi kwa uhuru huku akibainisha  kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Tanzania imepiga hatua kubwa, ikiwa imezipita nchi zaidi ya 50  kwa kuwa na uhuru wa vyombo vya habari.

Serikali Yataka Rudisho la Uwekezaji Lifikie Zaidi ya Asilimia 10

Serikali Yataka Rudisho la Uwekezaji Lifikie Zaidi ya Asilimia 10

Serikali inataka rudisho la uwekezaji ‘return on investment’ katika kampuni ambazo serikali inaumiliki wa hisa chache kuongezeka kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia zaidi ya asilimia 10  katika mwaka ujao wa fedha

Dhamira hiyo ilielezwa  Machi 28, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi  Dkt. Moses Kusiluka wilayani Kibaha, mkoani Pwani, wakati wa kufunga mkutano wa siku tatu wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali inaumiliki wa hisa chache. 

“Niwape changamoto ya kukuza rudisho la uwekezaji kutoka asilimia saba ya sasa kwenda zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka ili kufikia azma  hii mnapaswa kuongeza ufanisi wa utendaji," alisema.

alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, jumla ya uwekezaji wa Shlilingi  trilioni 86.3, umefanywa katika taasisi hizo, huku kati ya kiasi hicho Shilingi  trilioni 2.9 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache na Shilingi trilioni 83.4 ikienda kwa taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.   

Aidha, Balozi Kusiluka aliwapa changamoto wakurugenzi wa bodi za  kampuni ambazo ina hisa chache kuongeza ufanisi gawio kwa serikali.

 

Visitor Counter

000960
Today: 5
Yesterday: 3
This Week: 8
Last Week: 49
This Month: 112

Opening Hours

  • Monday: 8.30am–6.30pm
  • Tuesday: 10.00am–8.00pm
  • Wednesday: 8.30am–6.30pm
  • Thursday: 8.30am–7.00pm
  • Friday: 8.30am–3.00pm
  • Saturday: 8.30am–2.00pm
  • Sunday: 8.30am–2.00pm

Contact Us

Kanani A Road, Mumasama Street,

P.O.BOX, 137

Ngara, Tanzania

Mobile:  +255 744 172 741

Email: info@ishizwemedia.co.tz