Waziri Thabit Kombo Awasili  Nchini Uganda Kuwasilisha Ujumbe Maalum

Waziri Thabit Kombo Awasili Nchini Uganda Kuwasilisha Ujumbe Maalum

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mjumbe maalum, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Kampala Uganda na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Maj. Gen. Poul K Simuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe tarehe  Mei 12, 2025.

Waziri Kombo anatarajiwa kuwasilisha Ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Gen. Yoweri Kaguta Museveni.

Benki Kuu  Ukanda wa EAC Zahimizwa Kuweka Kipaumbele Katika Kutumia Rasilimali zao

Benki Kuu Ukanda wa EAC Zahimizwa Kuweka Kipaumbele Katika Kutumia Rasilimali zao

Benki Kuu katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) zimehimizwa kuweka kipaumbele katika kutumia rasilimali zao kwa ajili ya maendeleo yao, na kupunguza utegemezi kutoka nje.

Wito huo umetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania  Emmanuel Tutuba, katika Mkutano wa 28 wa Kamati ya Masuala ya Fedha (MAC) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Mombasa, Kenya.

Amesema nchi wanachama wa jumuiya hii zimebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi zinazofaa kutumiwa kwa maendeleo ya kanda hii. Ameeleza kuwa licha ya maendeleo ambayo yamepatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ukanda wa Afrika Mashariki unaendeleo kupitia changamoto nyingi za kiuchumi.

“Kumekuwa na kuongezeka kwa ushuru katika biashara, migogoro ya kimataifa na athari zinazotokana na tabianchi ambavyo vinahatarisha utulivu wa kiuchumi na jitihada za mtangamo,” amesema Gavana Tutuba.

Aidha, ametaja kukua kwa huduma bunifu za kifedha (fintechs) na fedha za kidigitali (cryptocurrencies), kama maeneo ambayo licha ya kuweza kuchangia kukua na ufanisi wa ujumuishi wa kifedha, yanaleta changamoto za usimamizi na uhalifu wa kimtandao.

“Hivyo, ushirikiano wa pamoja katika kuhakikisha uthabiti wa kifedha pamoja na kusaidia ukuaji wa endelevu wa kiuchumi ni muhimu. Lazima tushirikishane njia bora za utendaji, data, na uzoefu kwa jinsi tunavyofanya kazi pamoja na kujenga mazingira bora kwa kuchangia kukuza uchumi, ubunifu na uthabiti kikanda,"alisema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, Magavana na wawakilishi kutoka Burundi, Rwanda, Somalia, Kenya, Sudani ya Kusini, Tanzania na Uganda, walielezea maendeleo ya kiuchumi ya nchi zao, pamoja na utayari wao wa kuhakikisha masuala ya mtangamano katika sekta kifedha yanafanikiwa.

Mkutano huo, ulioanza Jumatano na kamati ya wataalam, umehitimishwa  Mei 9, 2025 na magavana chini ya uenyekiti wa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Dkt. Kamau Thugge. 

Mradi wa Maabara Tembezi za EAC Awamu ya 3 Yazinduliwa Rasmi

Mradi wa Maabara Tembezi za EAC Awamu ya 3 Yazinduliwa Rasmi

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameshiriki katika uzinduzi wa Awamu ya Tatu ya Mradi wa Mtandao wa Maabara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Mobile Labaratory Project Phase III) uliofanyika tarehe 9 Mei, 2025 katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha kando ya Mkutano wa 25 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo.

Mradi huo unaolenga kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na milipuko ya magonjwa na dharura za afya kwa njia ya uchunguzi wa haraka wa maabara sambamba na kuwajengea uwezo wataalam wa maabara katika nchi wanachama za EAC.

Viongozi wengine waliombatana na Dkt. Mollel katika uzinduzi huo ni: Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia masuala ya sayansi, Prof. Daniel Mushi, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe na maafisa waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na taasisi za Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar.

Aidha, katika awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huo Tanzania ilinufaika kwa kupata vifaa na mafunzo ya kitaalam, maabara mbili za afya zinazotembea (Mobile Laboratories) na kuimarisha mifumo ya taarifa na uhifadhi wa sampuli.

Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi wanachama kuimarisha mifumo ya afya ya kikanda ili kuyafikia malengo yaliyowekwa ya kuwazesha wananchi kupata huduma bora za afya na zenye uhakika.
 
Mbowe Hagombei Ubunge Wala Urais - Katibu Mkuu CHADEMA

Mbowe Hagombei Ubunge Wala Urais - Katibu Mkuu CHADEMA

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amesema amewasiliana na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama hicho Freeman Mbowe na ameeleza kuwa hana dhamira ya kugombea Urais, Ubunge au uongozi wa Chama chochote cha siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mnyika amesema “Natambua kuwa wachache waliojiondoa CHADEMA baadhi yao wamekuwa wakitumia jina lake kushawishi baadhi ya Viongozi wa Chama na wenye nia ya kugombea kujiondoa kwenye Chama kwa madai kuwa anawaunga mkono na anajiandaa kugombea Urais kupitia Chama kingine”

“Natambua pia mfumo wa Serikali na CCM uko nyuma ya baadhi yao kwa nia za kukwamisha no reforms no election, kupasua CHADEMA na kuhalalisha udhalimu na uharamu unaondaliwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025”

“Natambua kuwa mfumo huohuo ukihusisha Mtu wa karibu na Rais Samia Suluhu na Mtumishi mmoja wa Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ndio uliohusika kufungua kesi ya Said Issa Mohamed aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar na wenzake ambayo wameomba pamoja na mambo mengine shughuli za kisiasa za Chadema zizuiwe wakati kesi ya msingi ikiendelea”

“Kwa uzoefu wangu wa kuwa kwenye Sekretariati ya Chama kwa takribani miaka 21 mapito mengi ya CHADEMA ambayo tulifanikiwa kuyashinda, hii vita dhidi ya CHADEMA naamini pia tutaishinda, tuelekeze nguvu kwenye mapambano ya no reforms no election , tumjue vizuri adui yetu, tuwajue vizuri Washirika wetu, tuepuke kushambuliana sisi kwa sisi mpaka iwepo sababu ya kweli na ya lazima yakufanya hivyo, kwa umoja na nguvu ya pamoja, tutashinda”

Serikali ya Tanzania Yasisitiza Msimamo Wake wa Kudumisha Amani.

Serikali ya Tanzania Yasisitiza Msimamo Wake wa Kudumisha Amani.

Serikali ya Tanzania imesisitiza msimamo wake wa kudumisha amani, kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu 2025 unakuwa huru na wa haki na kulinda haki za msingi na uhuru wa Raia wote kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

Hayo yamesemwa kwenye taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyolenga kutoa ufafanuzi kuhusu maazimio yaliyopitishwa na Bunge la Ulaya May 08,2025 kuhusu kesi za kisheria zinazoendelea nchini “Huku Tanzania ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, Serikali inasisitiza tena msimamo wake usioyumba kwa kudumisha amani, kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, na kulinda haki za msingi na uhuru wa Raia wote kwa mujibu wa Katiba yake”

“Tanzania itaendelea kuweka nguvu kusimamia haki na heshima ya Watu wote kwa usawa kama Katiba inavyosema lakini ni muhimu kutoa ufafanuzi kwamba masuala yanayohusiana na mwelekeo wa kujamiiana yanashughulikiwa wazi ndani ya mfumo wa Katiba ya Tanzania, sheria za kitaifa, maadili ya kitamaduni, na kanuni za jamii, Tanzania inasisitiza tena kwamba ushirikiano wowote lazima uwe wa msingi wa kuheshimiana maadili, ikiwa ni pamoja na heshima kwa uhuru wa nchi, katiba, mifumo ya kisheria, na utambulisho, huku ushirikiano wa siku zijazo ukilenga vipaumbele vya pamoja katika maendeleo, utawala bora, ukuaji wa uchumi, ustawi wa Watu, na hali ya msingi ya maisha”

“ Tanzania inaendelea kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya na iko tayari kwa mazungumzo ya wazi, ya heshima na yanayotegemea ushahidi kuhusu masuala ya pamoja lakini mazungumzo haya lazima yawe ya msingi wa uwazi, haki, heshima ya pande zote, na uthamini kamili wa uhuru wa Taasisi za kila nchi, katiba, pamoja na muktadha wa kisheria na kitamaduni”

“Tanzania inakaribisha msaada unaoendelea kutoka Umoja wa Ulaya na Washirika wote wa kimataifa wanaojihusisha kwa nia njema na uelewa wa usawa wa wazi wa safari ya kidemokrasia ya nchi yetu na iko tayari kushirikiana na kuwapa uelewa zaidi wale ambao bado hawajafahamu maadili ya kitamaduni ya Tanzania”

Visitor Counter

000727
Today: 8
Yesterday: 4
This Week: 8
Last Week: 91
This Month: 210

Opening Hours

  • Monday: 8.30am–6.30pm
  • Tuesday: 10.00am–8.00pm
  • Wednesday: 8.30am–6.30pm
  • Thursday: 8.30am–7.00pm
  • Friday: 8.30am–3.00pm
  • Saturday: 8.30am–2.00pm
  • Sunday: 8.30am–2.00pm

Contact Us

Kanani A Road, Mumasama Street,

P.O.BOX, 137

Ngara, Tanzania

Mobile:  +255 744 172 741

Email: info@ishizwemedia.co.tz