Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka katika kukabiliana na biashara haramu ya Wanyamapori na mazao ya misitu inayovuka mipaka ya nchi ili kuboresha uhifadhi, kuendeleza utalii na kukuza uchumi.
Akifungua Mkutano wa 14 wa Kamati ya Wataalam wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka ulioanza Mei 06, 2025 Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Wanyamapori Dkt. Alexander Lobora amesema Mkataba huo umekuwa na manufaa makubwa kwa Nchi Wanachama kwa kuunganisha nguvu za pamoja kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
“Tumekuwa tukishirikiana na nchi nyingine kwa kupeana taarifa za kiintelijesia za wahalifu pale ambapo wanatenda kosa na kukimbilia nchi nyingine, au kuwa na washirika wa uhalifu katika mataifa mengine na kuchukua hatua za kuwakamata na kuwarudisha katika nchi walikotenda uhalifu ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.” Amesema Dkt. Lobora
Aidha Dkt. Lobora amesisitiza juu ya wananchi wanaojishughulisha na ujangili kuacha mara moja na kujielekeza katika kazi halali za kujipatia kipato kwa kuwa utekezaji wa mkataba huo hautaruhusu wahalifu kujificha popote.
Awali, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya Prof. Erustus Kanga ametoa rai kwa nchi za Afrika kushirikiana katika juhudi za kupambana na biashara haramu za mazao wanyamapori na misitu ikiwemo uwindaji haramu wa wa wanyamapori adimu wakiwemo faru kwa ajili ya vipusa na ndovu kwa ajili ya meno yao.
“Kupitia mkaba huu tungependa kuona Bara letu la Afrika hakuna mtu yeyote anayejihusisha na uwindaji haramu, wa Faru au Ndovu, atoe pembe Kenya ama atoe Tanzania na avuke mipaka ama, atoke Tanzania aende Zambia ama atoke Kenya aende kuziuza Kongo, hilo ndiyo jawabu letu kubwa kabisa. Tunataka kuona rasilimali zetu zinalindwa kwa kukomesha biashara haramu za mazao ya wanyamapori na misitu ili tuweze kunufaika na rasilimali zetu za asili.” Amesema Prof. Kanga
Mkataba wa Lusaka ulianzishwa mwaka 1994 Jijini Lusaka Zambia na Tanzania ni miongoni mwa mataifa sita yaliyoanzisha Mkataba na kuridhia utekelezaji wake mwaka 1996. Katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba, Tanzania itakabidhiwa kiti cha urais wa Baraza kwa kipindi cha miaka miwili kutoka Kenya.
.jpeg)

Serikali imesema vitambulisho vya Uandishi wa Habari (Press Card), vitaanza kutolewa wakati wowote baada ya siku saba kuanzia Mei 3, 2025 baada ya Waandishi wa Habari kuanza kujisajili rasmi kwenye mfumo wa TAI-Habari.
Mwandishi wa Habari ataanza kujisajili kupitia kiunganishi cha https://taihabari.jab.go.tz kisha kufuata maelekezo yaliyotolewa ili kukamilisha kujaza fomu yake kwenye mfumo huo wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
Kauli hiyo imetolewa Mei 3, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, katika Kijiji cha Sayu mkoani Shinyanga wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu masuala mbalimbali ya Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani humo.
“Tuliwaahidi kwamba tunawaletea Press Card (Vitambulisho vya kidijitali), ninayofuraha kuwajulisha kwamba 'press card' hizi za kidijital mchakato umekamilika, ziko tayari kwa matumizi, siku saba kuanzia sasa mtaingia kwenye kiunganishi cha Bodi ya lthibati ya Waandishi wa Habari na utaomba kitambulisho...," alisema Bw. Gerson Msigwa.
Alisema Mwandishi wa Habari akishajaza taarifa zake sahihi, Bodi itapokea maombi na kuyahakiki na kama yamekidhi vigezo kitambulisho kitachapishwa na kutumwa mahali alipo kupitia Klabu za Waandishi wa Habari katika maeneo yao.
“Ombi langu kwenu Waandishi wa Habari mtambue kitambulisho hiki ni mali ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania…, hivyo ukipewa wewe ndiye utakayewajibika kwa lolote litakalofanyika kwa utambulisho wa kitambulisho hiki, siyo kitambulisho umekiacha huko, mtu amekichukua kaenda kufanya utapeli tutambaini kwa sababu sasa tutakuwa tunaweza kufuatilia kwa kupitia mfumo, tukibaini tutakupata wewe,” alisema Bw. Msigwa na kuongeza;
“Ninachowaomba kitunzeni kama mboni ya jicho, huu ndiyo utambulisho wenu wa kazi, muwe nacho mfukoni, usikiache hovyo hovyo.”
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Wakili Patrick Kipangula, ili kurahisisha zoezi la kutuma na kupokea Press Card hizo, Waandishi wa Habari wanahimizwa kujisajili kwenye Klabu za Waandishi wa Habari zilizopo maeneo yao.
Wakili Kipangula alisema wakati wa kujisajili Waandishi wa Habari wanapaswa kuweka kwenye mfumo vyeti vilivyo halali na kwamba ikiwa Mwandishi ataweka cheti cha kughushi, Bodi ya Ithibati itachukua hatua kali za kisheria kwa sababu hilo ni kosa la jinai.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya uchochezi, amegoma kula akiwa gerezani kama ishara ya kutaka haki itendeke.
Wakili wa Tundu Lissu, Peter Kibatala amebainisha kuwa atasusua kula hadi pale atakapoona haki inatendeka ‘’Anaanza kususia kula chakula, sio kwasababu nyingine, anataka haki itendeke’’ alibainisha Kibatala wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Mbali na Shitaka la uhaini Tundu Lisu anatuhumiwa kwa kuchapisha taarifa za uongo kuhusu kuharibiwa kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, kutumika kwa Polisi kuipa kura na Majaji kutotenda haki kwa kuwa ni wateule wa Rais.
Lissu alikamatwa mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara mkoani Ruvuma, kusini mwa Tanzania mwezi uliopita wakati akiendelea kunadi msimamo wa chama hicho wa 'No Reforms, No Election, msimamo ambao ni wa kisera wa chama hicho uliopitishwa na Kamati Kuu katika kikao chake cha Desemba 2-3, 2024 unaodai kuwa CHADEMA haitoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama hakutafanyika mabadiliko ya kimfumo katika uchaguzi, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya katiba, sheria, na kuhakikisha kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na Maandalizi kuelekea sherehe za siku ya wafanyakazi Duniani zitakazofanyika kesho Mei mosi, 2025 kitaifa Mkoani Singida katika Uwanja wa Bombadia
Ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 30, 2025 alipopokea taarifa na kukagua maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe hizo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Majaliwa ameipongeza kamati inayoratibu sherehe hizo na kuwataka kuhakikisha wanakamilisha maeneo machache yaliyobaki ambayo yanahitaji maboresho.
Awali, akitoa taarifa ya maandalizi hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa na wapo tayari kumpokea Rais Dkt. Samia kwa ajili ya sherehe hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka, ametoa wito kwa wazazi, walimu, na watendaji wa kata kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni.
Amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya elimu na afya kwa watoto, hivyo ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuhakikisha suala hilo linapewa kipaumbele na kwamba hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa kila shule ina uwezo wa kuzalisha chakula chake, hivyo kuboresha lishe ya wanafunzi na kuongeza ufanisi katika elimu.
Shaka amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imejipanga kutumia rasilimali zilizopo, hususani ardhi yenye rutuba, kwa ajili ya kilimo cha chakula cha shule ambapo ametoa rai kwa watendaji wa kata ambao hawana maeneo ya kilimo kutoa taarifa ili wapatiwe ardhi kwa ajili ya shughuli hiyo muhimu.
Kikao hicho kimewashirikisha watendaji wa kata zote 40 pamoja na wataalam mbalimbali wa sekta ya lishe na elimu, DC Shaka amewataka watendaji hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuweka mkazo katika suala la lishe kwa wanafunzi huku akisisitiza kuwa agizo la kuhakikisha lishe bora kwa wanafunzi ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo ni lazima litekelezwe kwa vitendo.
Katika hatua nyingine DC Shaka ameahidi kuwa wilaya ya Kilosa itaendelea kumuunga mkono Rais kwa kuhakikisha kuwa suala la lishe kwa wanafunzi linapewa kipaumbele cha juu nakusema kuwa kwa kushirikiana na wazazi, walimu, na watendaji wa kata, watahakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata chakula cha mchana shuleni, hivyo kuboresha afya na ufaulu wao.