Dkt. Mollel Afanya Ziara ya Kukagua Kituo cha Afya Cha Mama Ngoma

Dkt. Mollel Afanya Ziara ya Kukagua Kituo cha Afya Cha Mama Ngoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amefanya ziara ya kukagua hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kukipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Mama Ngoma kuwa hospitali ya ngazi ya juu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mollel amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa, na amesisitiza umuhimu wa mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma kwa wananchi. “Tupo hapa kuhakikisha kilichoelekezwa na Waziri Mkuu kinatekelezwa kwa vitendo. Serikali haishindani na sekta binafsi bali tunashirikiana kutoa huduma bora kwa jamii,” amesema Dkt. Mollel.

Kwa upande wake, Profesa Ngoma ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa kituo hicho katika jamii na kukipa kipaumbele. “Hili si jambo kwa ajili ya mtu mmoja, ni kwa manufaa ya wananchi wote wa eneo hili na maeneo ya jirani,” amesema Profesa huyo..

Uwepo wa Hospitali ya Mama Ngoma katika eneo la Kwangoa umetajwa kuwa muhimu kutokana na umbali wa hospitali ya wilaya, hivyo kusaidia kupunguza gharama za Serikali na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Askofu Dkt. Shoo Aonya  dhidi ya Kurudia Makosa ya Chaguzi zilizopita atoa rai kwa Vyombo vya Dola Kutojiingiza Katika Upendeleo wa Kisiasa

Askofu Dkt. Shoo Aonya dhidi ya Kurudia Makosa ya Chaguzi zilizopita atoa rai kwa Vyombo vya Dola Kutojiingiza Katika Upendeleo wa Kisiasa

Katika ibada maalum ya Sikukuu ya Pasaka, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Fredrick Shoo, ametoa wito wa maridhiano ya kweli, uchaguzi huru na haki pamoja na kuheshimiwa uamuzi wa wananchi.

Akizungumza Aprili 20, 2025 katika Kanisa Kuu la Moshi Mjini, Askofu Shoo amesema,“tunaposema juu ya kuridhiana tunamaanisha, tunapotamka juu ya haki, amani na upeza leo ndo hatupaswi kuishia kwenye maneno tu ni lazima tuyatekeleze.”

Ameonya dhidi ya kurudia makosa ya chaguzi zilizopita, akitaka uchaguzi wa mwaka huu uwe wa wazi na unaoheshimu demokrasia huku akitoa rai kwa vyombo vya dola, kutojiingiza kwenye upendeleo wa kisiasa.

Aidha, amehimiza wananchi kuwa na hofu ya Mungu, kupenda nchi yao na kushiriki uchaguzi kwa ujasiri, wakiamini kuwa mabadiliko chanya yanawezekana.

Malawi yazuia  Kuingia Kwa Mazao ya Kilimo Kutoka Tanzania Waziri  Bashe atoa msimamo wake

Malawi yazuia Kuingia Kwa Mazao ya Kilimo Kutoka Tanzania Waziri Bashe atoa msimamo wake

Serikali ya Tanzania imesema imepokea taarifa rasmi kuwa Serikali ya Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi, na mahindi, hatua ambayo imeathiri moja kwa moja shughuli za Wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema hayo leo April 17,2025 kupitia ukurasa wake wa X ambapo amenukuliwa akiandika “Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio, hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka kumi katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda maslahi ya nchi yetu”

“Kutokana na hali hii, na baada ya juhudi zote za kidiplomasia kufanyika bila mafanikio, ninapenda kuwataarifu yafuatayo, iwapo Serikali ya Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao kufikia Jumatano ijayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili”

“Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa, usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na Wafanyabiashara wa Kitanzania”

“Wasafirishaji wote wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa za kilimo, ninawashauri kuacha kupakia bidhaa hizo mpaka hapo Malawi na Afrika Kusini watakapo badilisha msimamo wao, Wafanyabiashara walioweka order za apples, machungwa, na bidhaa zingine ambazo hununuliwa Afrika kusini, ninawashauri kuacha kwa sasa kwani hatutoziruhusu kuingia Tanzania mpaka hapo Afrika Kusini itakapo tufungulia soko la ndizi”

“Ninathibitisha kuwa kama Waziri mwenye dhamana, nimewasiliana kwa njia mbalimbali na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila mafanikio ya kupata majibu rasmi, hatUa hizi ni za kulinda heshima ya nchi yetu, uchumi wa wakulima wetu, na usawa katika biashara za kikanda”

Waziri Ndejembi amrejeshea mjane eneo lake, amwelekeza mkrugenzi  kuvunja  nyumba iliyojengwa kimakosa

Waziri Ndejembi amrejeshea mjane eneo lake, amwelekeza mkrugenzi kuvunja nyumba iliyojengwa kimakosa

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka za kuvunja nyumba iliyojengwa kimakosa katika kiwanja namba 1/31 kilichopo Block D, Iyumbu North jijini humo.

Waziri Ndejembi ametoa agizo hilo alipotembelea eneo hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa msimamizi wa mirathi wa familia ya marehemu Thobias Msigwa ambaye ni mmliki halali wa viwanja namba 1/30, 1/31, 1/32 na 1/33 kitalu D, Iyumbu North.

Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa mwenye hati halali ya kiwanja hicho ni msimamizi wa mirathi ya marehemu Thobias Simon Msigwa ambaye ni mke wake Prisca Lulambo.

Aidha, Waziri Ndejembi ametoa rai kwa watu kuacha kuvamia maeneo ya watu wengine ambayo yana umiliki halali na nyaraka halali katika Jiji la Dodoma na maeneo mengine nchini.

Zaidi ya Wakazi 12, 000 Wanufaika na Mradi wa Maji wa Mizani- Itete

Zaidi ya Wakazi 12, 000 Wanufaika na Mradi wa Maji wa Mizani- Itete

Zaidi ya wakazi 12,000 wa vijiji vya Alabama na Mizani, Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wameondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Mizani-Itete, unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025  ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 321, fedha zilizotolewa kupitia mpango wa "Lipa kwa Matokeo (PForR)."

Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Malinyi, Marco Chogelo, utekelezaji wa mradi wa Maji Mizani-Itete ulianza mwezi Februari 2024 na kukamilika mwezi Novemba mwaka huo huo.

Mradi huo umehusisha uchimbaji wa mitaro, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 8.2, ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba ya mitambo (power house) pamoja na ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lenye uwezo wa lita 200,000.

Wakazi wa Kijiji cha Mizani, Kata ya Itete, wamesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeimarisha shughuli zao za kiuchumi kwani awali walilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ali, aliipongeza RUWASA kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi wa vijijini.

“Niipongeze sana RUWASA kwa kazi kubwa mnayoifanya mmekuwa wakombozi wa wananchi katika suala zima la upatikanaji wa maji safi na salama vijijini” alisema kiongozi  huyo .

Visitor Counter

000727
Today: 8
Yesterday: 4
This Week: 8
Last Week: 91
This Month: 210

Opening Hours

  • Monday: 8.30am–6.30pm
  • Tuesday: 10.00am–8.00pm
  • Wednesday: 8.30am–6.30pm
  • Thursday: 8.30am–7.00pm
  • Friday: 8.30am–3.00pm
  • Saturday: 8.30am–2.00pm
  • Sunday: 8.30am–2.00pm

Contact Us

Kanani A Road, Mumasama Street,

P.O.BOX, 137

Ngara, Tanzania

Mobile:  +255 744 172 741

Email: info@ishizwemedia.co.tz