Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) leo Ijumaa Mei 16, 2025, wamefanya kikao na waandishi wa habari katika ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki zilizopo Dar es Salaam kwa lengo la kuutarifu umma kuhusu kuanza kushirikiana kuwapatia namba ya utambulisho (NIN) wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026.
Akiongea kwenye kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia, ameweka wazi kuwa namba ya utambulisho wa taifa itakuwa ni ya lazima katika kuomba mkopo kwa mwaka ujao wa masomo. “Tunatarajia kufungua dirisha la maombi ya mkopo mwezi Juni, 2025… kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 namba ya utambulisho wa taifa itakuwa hitaji la lazima katika maombi ya mkopo”, amesema Dkt. Kiwia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Bw. James Kaji, amesema kuwa NIDA wapo tayari kuwahudumia wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na kuomba mikopo kutoka HESLB kwa kuwapatia namba za utambulisho kwa wakati na hivyo wanafunzi wanapaswa kufika kwenye ofisi za NIDA mapema ili kupatiwa namba za utambulisho. “NIDA ni maisha, kwa sasa … NIDA inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mifumo yote ya serikali inasomana… tunawasisitiza waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kuhakikisha wanafika mapema NIDA ili kupata namba ya utambulisho wa taifa”, ameeleza Bw. Kaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya namba ya utambulisho kwenye uombaji mkopo. “Tayari wataalaamu wetu wa mifumo kutoka HESLB na NIDA wamekalimisha kuunganisha mifumo, ili kuhakikisha waombaji wote wa mikopo wanajaza namba za utambulisho katika maombi yao ya mkopo, na kupata taarifa za uhakika za waombaji mikopo ambazo pia zitasaidia katika urejeshaji wa mikopo”, amesisitiza Dkt. Kiwia
Kuhusu kurahisisha huduma kwa waombaji wa namba za utambulisho wa taifa, Bw. Kaji amesema NIDA imeboresha huduma kwa njia ya mtandao na kusisitiza waombaji wa namba za utambulisho wa taifa kuingia kwenye mtandao wa NIDA kwa kutumia kiunganishi https://eonline.nida.go.tz ili kuwasilisha maombi yao.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, ametembelea Makao Makuu ya Wakala wa Nishati Jadidifu wa Falme ya Morocco (MASEN) na kufanya mazungumzo na uongozi wa taasisi hiyo, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Tariki Ameziane Moufaddal.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco katika sekta ya nishati, hasa uzalishaji wa umeme na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Pande hizo mbili zimekubaliana kuteua wataalamu kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ili kuhakikisha manufaa kwa nchi zote mbili.
Bw. Moufaddal ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuimarisha miundombinu ya uzalishaji wa nishati. "Tanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika katika juhudi za kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa wananchi wote," amesema.
Londo aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Ali Mwadini, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, REA, TPDC na Wizara ya Mambo ya Nje. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kukuza ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu za maendeleo.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Kiongozi wa Comoro, Nour el Fatih Azali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili jirani.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu ya Comoro, Balozi Yakubu alieleza dhamira ya ubalozi kuandaa kongamano kubwa la Biashara na Uwekezaji mwezi ujao kwa kushirikiana na Serikali ya Comoro, likilenga sekta za uzalishaji, ujenzi na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
“Tunataka kuwahamasisha wawekezaji kutoka Tanzania na Comoro kushirikiana kikamilifu kwenye maeneo ya kipaumbele ya kiuchumi,” alisema Balozi Yakubu, huku akiwasilisha pia masuala mengine ya ushirikiano kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Kwa upande wake, Bw. Fatih aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na kufungua milango kwa taasisi za Tanzania kushiriki katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Comoro yatakayofanyika mwaka huu.
Kampuni ya Tembo Nickel Ltd imethibitisha ratiba ya kuanza rasmi ujenzi wa Mgodi wa Kabanga Nickel uliopo wilayani Ngara,Kagera.
Hayo yamesemwa leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lifezone Metals inayomiliki kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited kwa ubia na Serikali ya Tanzania, Ndg. Chris Showalter, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Kabanga Nickel kufuatia agizo lililotolewa na serikali la kutaka kampuni zote zenye Leseni za uchimbaji madini wa kati na kubwa kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa miradi husika baada ya kupata Leseni za uchimbaji Madini.
“Kampuni ya Tembo Nickel inathibitisha uendelezaji wa mradi wa Kabanga Nickel kwa mpango wa kuanza na uzinduzi rasmi wa ujenzi wa mradi(𝙜𝙧𝙤𝙪𝙣𝙙𝙗𝙧𝙚𝙖𝙠𝙞𝙣𝙜 𝙘𝙚𝙧𝙚𝙢𝙤𝙣𝙮) ifikapo mwezi Oktoba,2025. Sambamba na ujenzi wa mgodi huo,Kampuni inaendelea kuthibitisha mpango wake wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusafisha madini ya Nickel kwa kuyaongezea thamani ndani ya nchi”Amesema Showalter
Akizungumza katika kikao hicho,Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema Mradi wa Kabanga Nickel ni mmoja ya miradi mikubwa ambayo inategemewa kuleta mapinduzi makubwa katika kuchochea uchumi na maendeleo ya nchi yetu,hivyo “𝙘𝙤𝙢𝙢𝙞𝙩𝙢𝙚𝙣𝙩” iliyowekwa na Kampuni ya utekelezaji wa mradi ni muhimu kwa mustakabali ya ukuaji wa sekta ya madini na uchumi wa nchi.
Serikali imetoa wito kwa kampuni zote kuhakikisha zinaanza mara moja shughuli za uendelezaji miradi ya madini kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya madini sura ya 123, ni muhimu sheria kuzingatiwa katika utekelezaji wa miradi ili miradi hii ilete tija kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde amesisitiza Kampuni zote zenye Leseni za kati na kubwa kuhakikisha maeneo yao yanaendelezwa kwa mujibu ya masharti ya Leseni

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuongeza ubunifu kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa katika kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kupitia shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini sambamba na utoaji wa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Mhandisi Samamba ametoa kauli hiyo leo Mei 13, 2025 kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa makamishna wapya wa Tume ya Madini jijini Dodoma yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu Sekta ya Madini sambamba na majukumu ya Tume ya Madini.
Makamishna wapya walioteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan ni Mhandisi Theonestina Mwasha na Dk. Theresia Numbi.
Samamba amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini Aprili 2018 ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini umeongezeka na kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuwataka Makamishna wapya kuendelea kubuni mikakati mipya ya kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki kwenye shughuli za madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.
“Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana hususan ushiriki mkubwa wa watanzania kwenye Sekta ya Madini na kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, ninawataka kuongeza ubunifu hasa kwenye usimamizi wa eneo la utoaji wa leseni za madini, ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR) ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uendelee kukua.” Amesema.
Akielezea mafanikio katika Sekta ya Madini kwa kifupi, Mhandisi Samamba amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa 30, Maafisa Migodi Wakazi 13, Masoko ya Madini 43 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 109.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk. Janet Lekashingo amewapongeza makamishna wapya kwa uteuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuahidi ushirikiano kutoka kwa watendaji na watumishi wa Tume ya Madini.