RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh milioni 50 kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Maria Mtakatifu Mwana wa Mungu Kibwigwa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambapo kiasi cha Sh milioni 250.2 kilichangwa katika harambee hiyo.
Akitangaza matokeo ya harambee hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa ambaye mgeni rasmi alichangia Sh milioni 20. Amesema Rais Samia kwa mapenzi mema amechangia ujenzi huo baada ya kuombwa kufanya hivyo na askofu wa jimbo la Kigoma Mhashamu Askofu Mlola.
Kadogosa amesema kuwa katika harambee hiyo Rais Samia pia aliungwa mkono na Mwenyekiti wa kampuni ya GSM, Gharib Mohamed huku wapenzi wa timu za Simba na Yanga waumini wa kanisa hilo wakichangia kiasi cha Sh 890,000 ambapo wapenzi wa Yanga walichangia Sh 528,000 na wapenzi wa Simba Sh 362,000.
Awali Askofu wa jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola alimshukuru Rais Samia kwa mchango huo na kuongeza kuwa ni kiongozi anayejali watu kwa hali yeyote sambamba na kuwashukuru wote waliofaanikisha harambee hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema kwa mwaka 2025/26, itaongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kutoka 245,314 mwaka 2024/25 hadi wanafunzi 252,773.
Akiwasilisha leo bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2025/26, Prof.Mkenda amesema kwa mwaka wa kwanza watakaonufaika ni 88,320 na wanaoendelea 164,453 mwaka 2025/26.
Pia, amesema itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 10,000 wa ngazi ya stashahada katika fani za kipaumbele ikiwamo Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeanzisha majimbo mapya nane na kubadilisha majina ya majimbo 12 ya uchaguzi yatakayotumika kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo tarehe 12 Mei, 2025 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema Tume imefikia uamuzi huo baada ya kupitia maombi kutoka kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Ameyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Kivule amabalo limegawanywa kutoka Jimbo la Ukonga na Jimbo la Uchaguzi la Chamanzi ambalo limegawanywa kutoka Jimbo la Mbagala yote ya mkoani Dar es Salaam.
“Mkoani Dodoma limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Dodoma Mjini limegawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la Uchaguzi la Mtumba na Mkoani Mbeya limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Mbeya Mjini limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Uyole,” amesema.
Ameongeza kuwa Mkoani Simiyu limeanzishwa jimbo jipya moja ambapo Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la uchaguzi la Bariadi Mjini.
Jaji Mwambegele amesema Mkoani Geita yameanzishwa majimbo mawili ambapo Jimbo la Uchaguzi la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Katoro na Jimbo la Uchaguzi la Chato limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Chato Kusini.
“Mkoani Shinyanga limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Itwangi,” amesema.
Akizungumza kuhusu majimbo kumi na mbili (12) ya uchaguzi yaliyobadilishwa majina, Jaji Mwambegele ameyataja majimbo hayo kuwa ni pamoja na Jimbo la Uchaguzi la Chato ambalo limebadilishwa jina kuwa Jimbo la Uchaguzi la Chato Kaskazini.
“Jimbo la Uchaguzi la Nkenge limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Missenyi, Jimbo la Uchaguzi la Mpanda Vijijini limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Tanganyika na Jimbo la Uchaguzi la Buyungu limebadilishwa jina sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Kakonko,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tanzania Bara John Heche amewataka Wanachama wa Chama hicho kutotishwa wala kubabaishwa na walioshindwa mapambano na kuondoka kisa CHADEMA haishiriki uchaguzi bila mabadiliko kufanyika ambapo amesema Chama hicho kilianzishwa ili kuwaletea Watanzania mabadiliko na sio kutimiza ndoto za Watu kuwa Wabunge hata kupitia uchaguzi usio huru na haki.
Akiongea na Wakazi wa Sengerema Mkoani Mwanza leo Mei 12,2025, Heche amesema “No reforms no election ndio msimamo wa nchi, sasa wanaopotoka kuna wakati miongoni mwetu tulikuwa nao kwenye safari hii wameshindwa mapambano, wasitutishe, wanatuambia kwamba eti ndoto zao zinakatishwa kwa sisi kutoenda kwenye uchaguzi wa kuua Watu”
“Hiki Chama hakikuanzishwa kwa ajili ya ndoto ya Mimi Heche kuwa Mbunge, kilianzishwa kwa ndoto ya kuwaletea Watanzania mabadiliko, sio ndoto ya kukufanya uwe Diwani au Mbunge, hiki ni Chama cha ndoto ya Watanzania kurudisha nchi yao kwenye mikono yao, wasiwatishe, msibabaike, safari lazima iendele” amesema Heche

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mjumbe maalum, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Kampala Uganda na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Maj. Gen. Poul K Simuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe tarehe Mei 12, 2025.
Waziri Kombo anatarajiwa kuwasilisha Ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Gen. Yoweri Kaguta Museveni.