Serikali ya Tanzania Haingilii Kesi Mahakamani

Serikali ya Tanzania Haingilii Kesi Mahakamani

Serikali ya Tanzania imesema imeliona azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya May 08,2025 kuhusu kesi za kisheria zinazoendelea nchini lakini haijaridhishwa na hatua hiyo kwakuwa Bunge hilo limetoa maamuzi kwa kuzingatia taarifa za upande mmoja bila kushauriana kwanza kwa njia za kidiplomasia na Tanzania huku ikisisitiza kwamba Serikali haiwezi kuingilia Mhimili wa Mahakama.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema “Ingawa Tanzania inaheshimu uhuru wa kitaasisi wa Bunge la Ulaya na inathamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya bado inaona kuna umuhimu wa kufafanua baadhi ya mambo na kusisitiza wake wa muda mrefu kwenye maadili ya kidemokrasia, utawala bora, na utawala wa sheria”

“Tangu March 2021, Tanzania imefanya mageuzi ya kisiasa na kisheria chini ya falsafa ya 4Rs ambayo imezaa matokeo ya thabiti ikiwemo kurejesha uhuru wa kisiasa, upanuzi wa haki za raia, kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, na kupitishwa kwa sheria mpya za uchaguzi March 2024, ambazo zilisababisha kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi”

“Tanzania ni nchi huru yenye katiba yake na inatawaliwa na utawala wa sheria hivyo masuala ya kisheria yanashughulikiwa kwa uhuru na Mahakama kama moja ya Mhimili wa Dola kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ambapo Mhimili wa Serikali hauwezi kuingili kesi zinazoendelea Mahakamani, hivyo, kauli zinazohimiza Serikali iingilie utendaji katika kesi zinazoendelea za Mahakama sio tu hazifai lakini pia zinapingana na kanuni za msingi za uhuru wa Mahakama kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania”

“Tanzania ina wasiwasi na mwelekeo unaoendelea kama ulivyoonekana katika azimio la Bunge la Ulaya la baadhi ya Wadau wa kimataifa kutoa hukumu kwa kuzingatia taarifa zisizotosha au za upande mmoja, bila kushauriana kwanza kupitia njia za kidiplomasia, kesi za kisheria nchini zinachukuliwa kwa uchunguzi wa kipekee, pia maendeleo yaliyopatikana katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari, ushirikishwaji wa kisiasa, mageuzi ya uchaguzi, na ujenzi wa amani wa kikanda hayajazingatiwa kwenye maoni ya Bunge la Ulaya”

Tanzania Yadhamiria Kuendeleza Mageuzi ya Kidigitali Kwenye Elimu

Tanzania Yadhamiria Kuendeleza Mageuzi ya Kidigitali Kwenye Elimu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wadau wa elimu barani Afrika kuendeleza mkakati na ushirikiano utakaowezesha mageuzi ya kidigitali katika sekta ya elimu.

Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Mei 8, 2025 jijini Dar es salaam wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 18 la eLearning Afrika.

“ Tanzania inaendeleza dhamira yake ya mageuzi ya kidigitali katika elimu na tungependa kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wanazuoni ili kufanya e- learning kuwezeshwa kwa ghrama nafuu kwa wote ,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Tanzania imedhamiria kuongoza katika mageuzi ya kidigitali barani Afrika ambapo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inatambua kuwa mageuzi ya kidijitali ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na ushindani wa kimataifa. Ili kufanikisha hili, Tanzania imeandaa mifumo kadhaa ikwemo Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania 2024-2034.

Dkt. Biteko amesema kuwa Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali na Programu ya Tanzania ya Kidijitali zinalenga kuimarisha miundombinu na huduma za kidijitali, kuhakikisha teknolojia muhimu, vifaa, muunganiko na rasilimali za e-learning vinafika maeneo mbalimbali nchini, aidha nchi zingine pia zitumie rasilimali zao katika kusaidia mageuzi ya kidijitali katika nchi zao.

Airtel Africa Yatangaza Kufikisha Jumla ya Wateja Milioni 166.1

Airtel Africa Yatangaza Kufikisha Jumla ya Wateja Milioni 166.1

Kampuni ya Airtel Africa imetangaza kufikisha jumla ya wateja milioni 166.1 katika mataifa 14 ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, katika mataifa 14 ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, kulingana na tathmini iliyofanyika mwisho wa mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2025.

Idadi hiyo inaashiria ongezeko la asilimia 8.7, likichochewa na uwekezaji unaolenga kuimarisha ujumuishaji wa kidijitali na kupanua huduma za kifedha kupitia simu.

Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, wateja wa huduma za intaneti wameongezeka kwa asilimia 14.1 hadi milioni 73.4, huku matumizi ya data kwa kila mteja yakipanda kwa asilimia 30.4. Wateja wa huduma ya Airtel Money pia wameongezeka kwa asilimia 17.3 na kufikia milioni 44.6, huku thamani ya miamala ikifikia dola bilioni 145 kwa mwaka.

“Mkakati wetu unaoangazia uzoefu bora kwa mteja na upanuzi wa miundombinu umeendelea kuzaa matunda,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar. “Tumepanua mtandao wetu, kuboresha majukwaa yetu ya kidijitali, na kuongeza idadi ya vituo vya kutoa huduma ili kusaidia ujumuishaji wa kifedha.”

Licha ya changamoto za mabadiliko ya sarafu katika baadhi ya masoko, Airtel imetangaza faida ya dola milioni 328 baada ya kodi, tofauti na hasara ya dola milioni 89 mwaka uliopita. Kampuni pia imetangaza gawio la senti 6.5 kwa kila hisa kwa mwaka mzima.

EWURA Yatoa  Semina ya Udhibiti Katika Utekelezaji wa Miradi ya Gesi ya Kupikia

EWURA Yatoa Semina ya Udhibiti Katika Utekelezaji wa Miradi ya Gesi ya Kupikia

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mei 7 2025, imetoa semina ya Udhibiti katika utekelezaji wa miradi ya gesi ya kupikia, gesi asilia na CNG inayozalishwa nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ili wapate uelewa wa kina juu ya mwenendo na utendaji wa sekta hiyo yenye faida na manufaa kiuchumi nchini.

Akiwasilisha andiko lake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, ameeleza kuongezeka kwa hali ya ushindani katika biashara ya LPG kwa kuongezeka kwa makampuni yanayofanya biashara hiyo hali inayopelekea kuongezeka wa watumiaji wa nishati hii safi.

Kwa upande wa gesi asilia, Dkt. Andilile alisema, EWURA imetoa leseni 11 za vituo na biashara ya CNG na vibali vya ujenzi 22 vya miradi ya vituo vya CNG na kwamba 78% ya gesi asilia inatumika kuendesha vyombo vya moto na 22% viwandani.

“EWURA inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya LPG na CNG, kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha wanatumia nishati safi, kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli ambayo ni ghali na yenye madhara kwa mazingira kwa kuhamasisha matumizi CNG kwenye magari” alisema  Dkt. Andilile.

Wengine waliofanya wasilisho ni pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Tanzania Kuendelea Kushirikiana na Washirika Kudhibiti Ujangili

Tanzania Kuendelea Kushirikiana na Washirika Kudhibiti Ujangili

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka katika kukabiliana na biashara haramu ya Wanyamapori na mazao ya misitu inayovuka mipaka ya nchi ili kuboresha uhifadhi, kuendeleza utalii na kukuza uchumi.

Akifungua Mkutano wa 14 wa Kamati ya Wataalam wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka ulioanza Mei 06, 2025 Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Wanyamapori Dkt. Alexander Lobora amesema Mkataba huo umekuwa na manufaa makubwa kwa Nchi Wanachama kwa kuunganisha nguvu za pamoja kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.

“Tumekuwa tukishirikiana na nchi nyingine kwa kupeana taarifa za kiintelijesia za wahalifu pale ambapo wanatenda kosa na kukimbilia nchi nyingine, au kuwa na washirika wa uhalifu katika mataifa mengine na kuchukua hatua za kuwakamata na kuwarudisha katika nchi walikotenda uhalifu ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.” Amesema Dkt. Lobora

Aidha Dkt. Lobora amesisitiza juu ya wananchi wanaojishughulisha na ujangili kuacha mara moja na kujielekeza katika kazi halali za kujipatia kipato kwa kuwa utekezaji wa mkataba huo hautaruhusu wahalifu kujificha popote.

Awali, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya Prof. Erustus Kanga ametoa rai kwa nchi za Afrika kushirikiana katika juhudi za kupambana na biashara haramu za mazao wanyamapori na misitu ikiwemo uwindaji haramu wa wa wanyamapori adimu wakiwemo faru kwa ajili ya vipusa na ndovu kwa ajili ya meno yao.

“Kupitia mkaba huu tungependa kuona Bara letu la Afrika hakuna mtu yeyote anayejihusisha na uwindaji haramu, wa Faru au Ndovu, atoe pembe Kenya ama atoe Tanzania na avuke mipaka ama, atoke Tanzania aende Zambia ama atoke Kenya aende kuziuza Kongo, hilo ndiyo jawabu letu kubwa kabisa. Tunataka kuona rasilimali zetu zinalindwa kwa kukomesha biashara haramu za mazao ya wanyamapori na misitu ili tuweze kunufaika na rasilimali zetu za asili.” Amesema Prof. Kanga

Mkataba wa Lusaka ulianzishwa mwaka 1994 Jijini Lusaka Zambia na Tanzania ni miongoni mwa mataifa sita yaliyoanzisha Mkataba na kuridhia utekelezaji wake mwaka 1996. Katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba, Tanzania itakabidhiwa kiti cha urais wa Baraza kwa kipindi cha miaka miwili kutoka Kenya.

Visitor Counter

000960
Today: 5
Yesterday: 3
This Week: 8
Last Week: 49
This Month: 112

Opening Hours

  • Monday: 8.30am–6.30pm
  • Tuesday: 10.00am–8.00pm
  • Wednesday: 8.30am–6.30pm
  • Thursday: 8.30am–7.00pm
  • Friday: 8.30am–3.00pm
  • Saturday: 8.30am–2.00pm
  • Sunday: 8.30am–2.00pm

Contact Us

Kanani A Road, Mumasama Street,

P.O.BOX, 137

Ngara, Tanzania

Mobile:  +255 744 172 741

Email: info@ishizwemedia.co.tz